Katika
karne iliyopita, wasomi mbali mbali wakiwepo wanauchumi, pamoja na wataalamu wa
maswala ya kijamii waligundua umuhimu wa rasilimali watu katika kukua kwa
uchumi wa dunia. Kuwepo kwa elimu bora, na ujuzi katika nafsi ya binadamu huwasaidia
watu kujitengenezea vipato vikubwa. Tanzania inahitaji idadi kubwa ya rasilimali
watu ili iweze kupiga hatua kubwa za kiuchumi.
Kuwepo
kwa mali asili kama madini, mafuta na gesi asilia kwa kiwango kikubwa imekuwa
laana kwa mataifa kwani yamekuwa vyanzo vya unyanyasaji wa kijamii na umasikini
uliopitiliza kwa jamii zisizokuwa na rasilimali watu ya kutosha ili kuzisimamia
na kuziendeleza.
Baada
ya vita vya pili vya dunia, Ujerumani ilikuwa katika wakati mgumu wa kujinyanyua
kiuchumi. Miundombinu mingi iliharibiwa kipindi cha vita. Na Ili kujinyanyua
kutoka katika uharibufu mkubwa uliosabishwa na vita, serikali ya Ujerumani ilibuni mfumo wa elimu
ambayo ilielekeza juhudi zake katika kutayarisha rasilimali watu. Elimu
ilipewa kipaumbele; Ilifanywa kuwa ya bure na ya lazima kwa kila mjerumani.
Mfumo huu wa elimu ulifanywa kuwa wa vitendo zaidi na lazima kwa kila mtoto
mwenye umri wa miaka tano hadi kumi na tisa, huku kila mwanafunzi akipewa
nafasi kuchagua cha kujifunza kutokana na uwezo wake lengo kubwa ikiwa ni
kutayarisha rasilimali watu.
Jitihada
hizi za serikali ya Ujerumani ilizaa matunda makubwa ambayo yaliitwa miujiza ya
kiuchumi. Leo, uchumi wa Ujerumani ndio uchumi mkubwa zaidi katika bara la
Ulaya, na pia ndio mdhamini mkubwa wa mataifa taabani kiuchumi kama Ugiriki,
Hispania nk. Ujerumani ni moja ya mataifa yaliyo juu zaidi kwenye maswala ya
uhandisi inaongoza kwa uhandisi. Ujerumani inaongoza kwa uzalishaji wa viwanda
ikiuza nje ya nchi bidhaa yenye thamani ya dola za kimarekani trillion 1.52 kwa
mwaka 2012 tu. Haya ni mafanikio yaliyotokana na kuipa elimu kipaumbele, pamoja
na matumizi ya rasilimali watu zilizoko ndani na nje ya nchi.
Mataifa
yasiyokuwa na mali asili nayo yameonyesha ubunifu wa hali ya juu. Israel kwa
mfano, ni taifa dogo lenye rasilimali chache, huku ikizungukwa na maadui ambao
lengo lao kubwa ni kuliangamiza. Ikiwa imezingirwa na maadui kila kona pamoja
na kukosa rasilimali za asili, Israel imelazimika kutumia rasilimali watu ili
isiangamizwe kijeshi na kiuchumi.
Licha
ya kujitengenezea baadhi ya taasisi bora za kielimu na utafiti duniani, Israel
iligeukia wataalamu wenye asili ya kiyahudi waliotapakaa katika kila pembe ya
dunia, ikiwapa uraia watu wote wanaotaka kurudi nchini humo. Leo Israel ndio
moja ya nchi iliyoendelea zaidi kiteknolojia. Vyuo vikuu vya Israel vimezalisha
wataalamu wa kila aina ambao wanasaidia
nchi hiyo kujiendeleza kiuchumi na kujilinda kijeshi.
Baada
yakugundua kwamba hatma yake haikuwa nzuri kiuchumi na kijamii, Singapore, nchi
ndogo barani Asia ilianzisha mapinduzi ya miundombinu , viwanda, mawasiliano,
na ya kielimu ili iweze kustahimili mabadiliko ya kiuchumi ya baadae. Leo,
Singapore ni nchi ya nne duniani kwenye maswala ya kifedha na mmoja wa magwiji
katika masoko yanayochipukia. Korea kusini nayo haina tofauti na Singapore,
kwani ilikuwa masikini zaidi ya Kenya mwaka 1960. Leo hii Korea ya Kusini ina
uchumi wenye thamani ya dola za kimarekani trillion 1.56 ambayo ni mara 47 ya
Kenya. Hii yote imetokana na jitihada zake za kuzalisha rasilimali watu.
Marekani
imekuwa ni taifa lenye nguvu zaidi ya nchi yoyote ile duniani kiuchumi,
kiteknolojia na kijeshi. Kwa kipindi kirefu sasa. Mapinduzi ya viwanda ya karne
ya 19 iliisukuma nchi hiyo kutumia kila mbinu ; Marekani ilitumia rasilimali
zake zote ikiwemo rasilimali watu. Mafanikio ya taifa hili kubwa duniani
hayakuwa ya kubahatisha, yametokana na kufanya kazi kwa bidii bila kukata
tamaa, na pia kujivunia kile wanachokifanya.
Wamarekani
wamewekeza kwenye elimu kwa kiwango kikubwa. Wameanzisha vyuo vikuu vya elimu
na utafiti bora kuliko zote duniani. Sera zao za uhamiaji zimekuwa kivutio kwa
wataalamu bora kutoka kila pembe ya
dunia ili tu watu wenye vipaji waendelee kusadia taifa hili kuendelea kuongoza
kiuchumi. Hazina kubwa ya Tanzania imetapakaa ulimwenguni. Wataalamu mbali
mbali wenye asili ya kitanzania wametapaa kila pembe ya dunia wakitafuta maisha
huku wakichangia maendeleo ya mataifa mengine kutokana na kukosa uhuru wa
kuchangia nchi yao ya kuzaliwa.
Wataalamu
wenye asili ya Kitanzania wapo katika taasisi kubwa za kitafiti nchini marekani
na mataifa mengine makubwa; wapo kwenye mashirika makubwa ya kifedha, wapo
kwenye taasisi kubwa za afya nk. Mifano ni mingi ambayo siwezi kuielezea yote
kwa leo, ila lengo langu ni kuielemisha jamii yetu kuhusiana na umuhimu wa
watanzania waishio ughaibuni
Ushindani
mkubwa wa kiuchumi katika eneo la maziwa makuu ni msukumo tosha kwa Tanzania
kutumia kila mbinu inayoweza kuwa mstari wa mbele tukizingatia kwamba, Tanzania
ni moja ya nchi chache barani Afrika yenye utajiri mkubwa; kwani imebarikiwa na
kila aina ya rasilimali muhimu ambazo zingesaidia kuharakisha maendeleo yake.
Ugunduzi wa gesi asilia na mafuta, madini pamoja na mbuga zake za wanyama ni
rasilimali adimu na muhimu kulikwamua
taifa kutoka katika wimbi la umasikini.
Kinachohitajika
ni rasilimali watu; Kinachohitajika ni wataalamu wenye asili ya kitanzania
waliopo ndani na nje ya nchi kushirikiana ili kuleta maendeleo ya haraka.
Lazima watu wote wenye asili ya Kitanzania wapewe haki yao ya kikatiba pamoja
na nafasi ya kushiriki kulijenga taifa, kijamii, kiuchumui na kisiasa
Kamwe
Tanzania haiwezi na haitaweza kuendelea ikitegemea wageni. Watakaoleta
maendeleo na mabadiliko makubwa ni watanzania wenyewe. Mipaka ya dunia
imefunguka katika hii karne ya ishirni na moja. Badala ya kukumbatia misaada
inayotudhalilisha na wageni wanaoiba rasilimali zetu, tutumie hazina kubwa
tuliyonayo ya rasilimali watu, ili
tuweze kujikwamua kutoka katika wimbi la umasikini.
Wataalamu
wa kitanzania waliotapakaa duniani, wanastahili haki ya kurudi kwenye ardhi yao
ya kuzaliwa bila vikwazo vya aina yoyote. Katika kuandaa katiba mpya ya
Tanzania, tusifanye kosa la kuwafungia nje ndugu zetu walio ughaibuni kwa kuwa na
vibali vya kuishi na kusafiri. Ikumbukwe kwamba, pamoja na kuwa na vibali hivyo, bado asili
zao na mioyo yao itabaki Tanzania. Tusiruhusu historia ituhukumu hasa katika
kipindi hiki ambapo ushindani wa maendeleo ya kiuchumi unazidi kuongezeka
duniani
Mungu
Ibariki Tanzania
John Mashaka
Mashaka.john@yahoo.com
Mashaka.john@yahoo.com
Comments