Wakati Lissu akiendelea na ufafanuzi huo, baadhi ya wajumbe walianza kunong’ona kuwa TBC imesitisha matangazo.PICHA|MAKTABA
Na Sharon Sauwa na Editha Majura, Mwananchi
Dodoma. Shirika
la Utangazaji Nchini (TBC) jana limevuruga mwenendo wa Bunge la Katiba
baada ya kukata matangazo yake wakati mjumbe wa Bunge la Katiba, Tundu
Lissu alipotoa ufafanuzi wa maoni ya walio wachache.
Mgogoro
huo ulitokea bungeni jana wakati Tundu Lissu akitoa ufafanuzi kuhusu
maoni ya wajumbe walio wachache wa kamati namba nne.
Wakati Lissu akiendelea na ufafanuzi huo, baadhi ya wajumbe walianza kunong’ona kuwa TBC imesitisha matangazo.
Hata hivyo, kauli hiyo ilimfanya Lissu kudharau na kuendelea na ufafanuzi wake.
Baada
ya muda mfupi alisimama mjumbe wa Bunge hilo, Freeman Mbowe na kuomba
mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge hilo kuhusiana na tukio hilo.
“Mjadala
huu ni muhimu sana na mjadala huu umekuwa ukirushwa na kituo cha
televisheni cha Taifa TBC muda wote tangu tumeanza. Hivi punde kuna
taarifa kuwa TBC wamekata matangazo yote ya Redio na Televisheni una
nini cha kuwaeleza Watanzania?”alihoji Mbowe.
Akijibu
mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, alisema taarifa
ya TBC kufunga matangazo ni ya kushtua sana kwa sababu Bunge Maalumu
lina mkataba na serikali pamoja na TBC One wa kuhakikisha mjadala na
matangazo yote ya Bunge hilo yanaonekana na kuwafikia wananchi.
“Naomba
Katibu achunguze mara moja, aangalie nini kimetokea kama ni tatizo la
muda ama la kiufundi na tutapata majibu sasa hivi,”alisema na kulazimu
Bunge hilo kusimama kwa muda.
Baada muda mfupi, Sitta alisema tatizo ni hali ya hewa jijini Dar es Salaam.
“Katibu
amepanda huko juu katika studio na maelezo ya kitaalamu yanasema hali
ya hewa Dar es Salaam,” alisema kauli iliyoamsha kelele kutoka kwa
baadhi ya wajumbe hao huku wengine wakisikika wakisema barabara
zimekatika na uwanja wa ndege umefungwa jana.
Hali hiyo ilimbidi Sitta kuwasihi wajumbe hao kutulia kwa sababu mambo yote yangetengezwa.
“Ni
hivi kwa sababu yoyote ile hatuwezi kuendelea,” Hali hiyo iliibua
nderemo na vifijo kutoka kwa baadhi ya wajumbe huku wakitamka “Sitta,
Sitta, Sitta.”Chanzo.Mwananchi
Comments