ILE SINEMA YA TUMBILI NA MWIZI ILIYOCHEZWA NA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI NA MBUNGE WA NCCR-MAGEUZI KUMBE NI YA BURE LAKINI NI HATARI SANA KWA WATANZANIA !!!.

VIONJO VYA WIKI: Hakika Jaji Werema, Kafulila mmetuonyesha sinema ya bure, ambayo ni hatari.

Na Ndyesumbilai Florian, MCL.

Tukio kama hili laiti lingekuwa la utani baia ya Mhaya na Mkurya, ambao siku zote ni watani wa jadi, ungeweza kuvumiliwa na hakuna ambaye angejali.

Kwa bahati mbaya, hiki kilichotokea baina ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila ni aibu.


Ninaamini kama ingekuwa ni utani baina ya Mhaya akimshambulia Mkurya, ingewezekana mmoja wao akasimama hadharani bila woga au hofu na kusema, nambo unisamehe mtani, mimi nilikuwa natania.


Nilikuwa natania tu kwani huyu ni mtani wangu, naomba anisamehe, bila shaka mambo yote yangeishia hapo na wangeondoka kwenda kula au kunywa pamoja kule Mnadani, tena wote wakicheka kana kwamba hakukuwa na jambo lolote baina yao.


 
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu (kushoto) akijaribu kuwasuluhisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema (kulia) na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila katika Viwanja vya Bunge Dodoma hivi karibuni. Picha na Edwin Mjwahuzi.


Nasema kama ungekuwa utani baina ya watu wa makabila hayo mawili kutoka Kanda ya Ziwa au ilivyo kwa Mchaga na Mpare, kule Kaskazini, sidhani kama tungefika huko na hata kuona yote abayo yameendelea.


Lakini, kwa bahati mbaya wawili hao ambao pia ni watani, ni wawakilishi wa watu kwa namma moja au nyingine, ingawa wanatokea kwenye njia tofauti, inafaa wajiangalie.


Ninasema wazi bila kificho kuwa hata kiwajihi au maumbile wawili hao hawafanani, kukaribiana hata kidogo, wao kwa hakika wamekwenda mbali sana. Tumeambiwa wanatishiana maisha.


Tumeambiwa kwa siku mbili kwamba wametengeneza uhasama ambao ni hatari licha ya kuwa wao walianzia mashambulizi baina yao kwenye kuitana mmoja mwizi na mwingine tumbili, lakini hatimaye hasira zikawapanda.


Sioni kama mtu kuitwa tumbili, yeye kama binadamu anaweza kubadilika kesho yake na kuota manyoya, mkia, kuishi vichakani kama ilivyo kwa wanyama hao akila mahindi mabichi.


Pia, sidhani kama mtu ni mwadilifu kweli, ameishi na kufanya kazi bila dosari, si mdokozi wa mali za umma, kama mtu aliyeitwa mwizi, bila shaka angedharau na kisha kusonga mbele.


Ninajiuliza, uko wapi uvumilivu wetu ambao tumejinadi nao kwa miaka mingi kwamba sisi (Watanzania) ni wapole, watu wa amani, mshikamano.


Kadhalika, ninajiuliza, zinasema nini kanuni za Bunge ambazo zinasimamia taratibu za mijadala na hasa baada ya kuona ofisi hiyo imekaa kimya, haitoi karipio au onyo dhidi ya wawili hao, hasa kwa mfano ambao ninadiriki kusema kuwa ni mbaya.


Huu, unaweza kuonekana kama mzaha, ambao umeanzia kwa Jaji Werema na Kafulila, lakini unaweza kwenda mbali zaidi siku nyingine ambazo siyo nyingi na kuwahusisha watu wengine endapo busara zitaendelea kukosekana, ipo siku tutawaona wakidiriki kuvaana maungoni au kupigana na vyombo vya habari kama runinga vikiwaonyesha laivu.


Kama tatizo litakuwa ni kwenye kanuni za Bunge ambazo pengine zimekuwa kimya hazisemi au hata kutoa adhabu kwa wale wanaokiuka taratibu zikiwamo za kutoleana maneno makali, maudhi, basi inafaa ziangaliwe upya ili kuepusha aibu inayoweza kujitokeza katika jengo hilo ambalo siku zote huwa naliita kiota.


Ninadhani kamati ya maadili na hadhi ya wabunge ina jukumu la kuchukua hatua dhidi ya wale ambao wanadhihirika kukosa staha, nidhamu kama tukio la Jaji Werema na Mbunge Kafulila linavyojaribu kutuonyesha hapa.


Wawili hao, ambao wote naamini ni waumini wa Kikristo, ambao wana hofu ya Mungu, nawashauri warejee swali aliloulizwa Yesu, nimsamehe mara ngapi ndugu yangu aliyenikosea hata saba mara saba? Yeye (Yesu) alijibu kuwa si saba mara saba, bali saba mara sabini?


Ninasema neno samahani inaelekea ni gumu na ndiyo maana limekosekana siyo kwa wawili hao bali tulio wengi, ndiyo maana tumefikia mahali pa kuona wawili hao hawako tayari kwa suluhu, ingawa ninafarijika kuona watu wenye busara wakijaribu kuwapatanisha.


Ni imani yangu kuwa mbele ya safari, mfano huu mbaya na potofu wa Jaji Werema na Kafulila kule Dodoma hautajitokeza tena.


Ni vyema viongozi wetu wakajitambua kuwa wao ni viongozi, ni watu ambao wanabeba dhamana kubwa mele ya jamii inayowatazama.


Wakumbuke kuwa wao wanaonekana kama kioo iwe kwa matendo, maneno yao, hivyo wao kuanza kutishana, kushambuliana kwa iwe matusi au mambo mengine ni mambo ambayo ninasema kuwa hayakubaliki, hayafai kuendelea hata kidogo.


Kitendo cha Jaji Werema, kwa mfano kutokuwa tayari hata kupeana mkono na Kafulila mbele ya msuluhishi, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan ‘Zungu’ kinaashiria nini zaidi ya chuki kali ambayo kiongozi huyo ameijenga dhidi ya mbunge huyo?


Hili ni jambo ambalo kwa jumla halivutii, halipendezi hata kidogo kuendelea kufanywa na viongozi kama wao. Inafaa liachwe.


Ni wazi kwamba vitendo kama hivi vinaashiria jambo moja, kwamba inawezekana mara zote wabunge wetu wanapokuwa Dodoma, kumbe wanajisahau.


Sasa, tunaona hofu aliyona nayo Kafulila kwamba huenda anaweza kushambuliwa, kudhuriwa kama ambavyo imewahi kuwatokea watu wengine katika jamii ni ushahidi kwamba wanafanya mambo, kumbe wana hofu.


Hofu hiyo imetokea baada ya Jaji Werema kukaririwa juzi akisema kuwa atamshughulikia, jambo ambalo linaonyesha kumbe mizaha hutumbuka usaha.


Ninaishauri ofisi ya Bunge kuwa lazima iwe macho zaidi, makini, iamke kutoka kwenye usingizi huu wa kufikiri kuwa kila jambo litakwenda na kupita kiurahisi tu na kama wamepokea malalamiko ya wawili hao wayatolee uamuzi ambao utafahamika wazi na jamii kwa jumla wake na wala isiwe siri.


Tukio hili la Jaji Werema na Kafulila limefichua mambo mengine mengi ambayo awali nayo yalikuwa yakifichwa kiasi kwamba kumbe baadhi ya wabunge wetu siyo waadilifu, hawana nidhamu, hawaheshimiani wao kwa wao.


Hivyo, ushauri wangu kwao ni kuwa wabunge ambao ni watu wazima, wasomi waliobobea hawana budi kuwa makini zaidi na hasa lugha zao zile ambazo wanazitumia katika kuzungumza, wajifunze kujenga hoja, kwa umakini, uadilifu mkubwa. Ninasema umakini zaidi unahitajika kwa sasa kuliko ilivyo mazoea kwa wengi, ambako baadhi ya viongozi wetu wamekuwa wakiongozwa na jazba, itikadi na hata ushabiki wao kisiasa, kuliko kuzingatia hali halisi.


Kwa hiyo, inafaa wabunge wetu wote, wanaume kwa wanawake, wao wasisahau kuwa ni viongozi wa watu. Kwanza, wajitambue wao na wajibu wao, kisha wawe makini katika ndimi zao, watulivu katika mioyo, nafsi zao, wavumiliane na kamwe wasijaribu kuwaudhi, kuwachokoza wenzao. Pia watambue kuwa wakifanya hivyo hawana budi kuomba msamaha na kinyume chake wanajidhalilisha wenyewe tena kwa kiasi kikubwa mbele ya jamii.


Hivyo, ni vyema wabunge wetu wote wa majimbo, kutuliwa au viti maalumu wabadilike, wajitambue zaidi wao kama viongozi wa watu, pia waishi kwa kuongozwa na uadilifu, wakiamini kuwa wao ni watumishi wa watu.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.