JK;SAIDIENI KUONDOA UMASIKINI KWA WANANCHI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amezitaka taasisi za Serikali kuongeza kasi ya kupunguza umasikini miongoni mwa wananchi, akisisitiza kuwa wananchi wamekaa katika umasikini kwa muda mrefu mno kupita kiasi.   

Rais Kikwete amesema kuwa wanachotarajia wananchi kutoka kwa taasisi za Serikali ni kusaidiwa kutoka kwenye umasikini kwa kasi kubwa zaidi kwa sababu wamekaa katika hali ya umasikini kwa muda wa kupita kiasi.   
Rais Kikwete ametoa maelekezo hayo leo, Jumapili, Julai 20, 2014, wakati alipokagua shamba la kisasa la zao la buni kwenye kijiji cha Lipokela, Wilaya ya Songea, ikiwa ni moja ya shughuli zake katika siku ya nne ya ziara yake ya siku sita katika Mkoa wa Ruvuma.

Rais Kikwete amesimama kwenye shamba hilo akiwa njiani kutoka Wilaya ya Mbinga kuelekea Wilaya ya Songea ambako leo amefungua soko la kimataifa katika kijiji cha Mkenda, kilicho mpakani kabisa mwa Tanzania na Mozambique. Baadaye, Rais amekagua daraja kwenye Mto wa Ruvuma ambalo linaunganisha Tanzania na Mozambique.

Rais Kikwete ametoa maelekezo hayo baada ya kuambiwa kuwa pamoja na kwamba shamba hilo, pengine ni kubwa kuliko jingine lolote la buni nchini, limefanikiwa kupata miche 3,000,000 ya buni za kisasa ambayo lilihitaji lakini wakulima wa kawaida wa zao hilo la kahawa wanashindwa kupatiwa kiasi hicho hicho cha miche ya buni.

“Kwanini tunashindwa kupata miche milioni tatu kwa ajili ya wananchi ambayo wenyewe mmesema kuwa gharama yake yak uizalisha ni shilingi milioni 900? Kwanini tunashindwa kupata miche ya kutosha ili wakulima wetu wapande na kuongeza kipatoc hao?”Rais Kikwete amemwuuliza Profesa James Teri, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Kahawa Tanzania (TACRI).
Ameongeza Rais Kikwete: “Hatuwezi kuwabakiza wananchi wetu katika umasikini kwa miaka mingine 30 kwa sababu tu hatuna uwezo wa kuzalisha miche ya kutosha. Hatuwezi kufanya hivyo, wameishi kiasi cha kutosha katika umasikini.”
   
Amesisitiza Rais Kikwete: “Kazi yetu ni kuwatoa watu wengi zaidi katika umasikini kwa haraka kubwa zaidi kwa sababu wamechelewa mno. TACRI inaweza kufanya hivyo kwa kuwapa wananchi mbegu bora zaidi ya buni, ili waondokane na mibuni ya zamani ambayo uzalishaji wake ukochini. Hivyo, nataka kujua tunaweza kufanya nini kufanikisha hili siyo kuniambia habari ya changamoto ambazo TACRI inakumbana nazo katika kutimiza majukumu yake.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Siridhiki na kasi ya kujaribu kuwatoa watu wetu katika umasikini. Nahitaji kupata miche milioni tatu kwa ajili ya wananchi wetu. Kama iliwezekana kulipatia shamba hilo miche milioni tatu kwa nini isiwezekane kwa wananchi?”

    Shamba hilo kubwa la mibuni (inayozalisha kahawa) ni mali ya Kampuni ya AVIV, ambayo ni kampuni tanzu ya Kampuni ya Olam International, ambayo inaendesha shughuli za biashara katika nchi 65 duniani.

Olam iliingia Tanzania miaka 20 iliyopita na shughuli zake kubwa ni katika mazao ya korosho na kiwanda cha kuchambua pamba kilicho Bunda, Mara.

Duniani, Olam ina mashamba ya mibuni katika nchi tano ambazo ni Tanzania, Zambia, Ethiopia, Laos na Brazil.

AVIV ambayo inapanda mibuni ya kuzalisha kahawa yaa ina ya Arabica ilipanda miche ya kwanza miaka mitatu iliyopita na inakaribia kuvuna kwa mara ya kwanza. Katika kijiji hicho cha Lipokela, AVIV ina ardhi yenye ukubwa wa hekta 2,000.
Rais Kikwete anaendelea na ziara yake katikaMkoa wa Ruvuma leo kwa kutembelea na kukagua shughuli za maendeleo katika Wilaya ya Namtumbo.

Mwisho!

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
20 Julai,2014

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.