Maalim Seif afutarisha na kutembelea wagonjwa Donge

 



Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwasili katika kijiji cha Donge Muwanda kufutari na wananchi wa kijiji hicho.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akijumuika na wananchi wa kijiji cha Donge Muwanda katika futari ya pamoja.
Mzee Abdulhakim Muhsin Abeid wa kijiji cha Donge Muwanda, akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho baada ya kufutari  pamoja  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiitikia dua baada ya kumjuilia hali mzee Foum Denge (kushoto) wa kijiji cha Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwafariji baadhi ya wananchi katika ziara yake ya kutembelea wagonjwa na wafiwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiagana na wazee mbali mbali katika kijiji cha Bumbwini, baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea wagonjwa na wafiwa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja. (Picha zote na Salmin Said, OMKR)


Na Hassan Hamad OMKR

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amejumuika pamoja na wananchi wa kijiji cha Donge Muwanda katika futari ya pamoja aliyoiandaa kwa ajili ya wananchi wa kijiji hicho.
 
Akitoa nasaha zake baada ya futari hiyo, Maalim Seif amewahimiza wananchi wa Donge kuendeleza umoja na mshikamano walionao, na kamwe wasikubali kugawanywa kwa sababu zozote zikiwemo za itikadi za kisiasa.
 
Maalim Seif ambaye baada ya futari hiyo aliungana na waumini wa kijiji cha Donge katika sala ya Isha na Tarawehe, amewasisitiza wananchi hao kuendeleza utamaduni wa kufutari pamoja ambao uliasisiwa tokea wakati wa enzi za Mitume, na kwamba kufanya hivyo kutakuza mshikamano na mapenzi miongoni mwao.
 
Amewashukuru wananchi hao wa Donge Muwanda kwa kukubali kuungana nae katika futari hiyo, kitendo ambacho amesema kimempa faraja na matumaini ya kuendelea kwa mshikamano uliopo nchini.
 
Mapema akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Donge Muwanda, Mzee Abdulhakim Muhsin Abeid, amempongeza Maalim Seif kwa uamuzi wake wa kufutari na wananchi wa kijiji hicho.
Amesema kitendo hicho kimewaleta pamoja wananchi mbali mbali wa kijiji hicho, na kuomba utamaduni huo uendelezwe ili kukuza mshikamano na maelewano miongoni mwa wananchi.
 
Akizungumzia kuhusu historia ya kijiji hicho cha Muwanda, Mzee Abdulhakim amesema kijiji hicho kina historia ndefu tokea wakati wa ukoloni na harakati za kupigania uhuru.
 
Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amefanya ziara ya kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa na wafiwa katika vijiji mbali mbali vya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
 
Katika ziara hiyo Maalim Seif amewatembelea wagonjwa na kuwafariji wafiwa katika vijiji vya Matemwe, Donge, Kitope na Bumbwini, ambapo anatarajiwa kuendelea na ziara hiyo kwa Mikoa yote ya Unguja na Pemba, ndani ya kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*