MKE WA ASKARI WA JESHI LA POLISI AFARIKI DUNIA MWEZI WA RAMADHANI AKIWA KATIKA CHUMBA CHA MWENDESHA PIKIPIKI MAARUFU BODABODA MJINI MOSHI.


Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga.

Moshi.
 

Jeshi la Polisi linamshikilia dereva mmoja wa pikipiki, maarufu kama bodaboda wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro baada ya mke wa askari polisi kukutwa amekufa chumbani kwa dereva huyo.

Tukio hilo ambalo limezua gumzo kubwa wilayani humo lilitokea juzi saa 12:00 jioni katika eneo la New Mwanga wilayani humo na mtuhumiwa akidaiwa kukutwa akiwa amelewa chakari.


Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea.


“Hilo tukio lina ukweli na bahati mbaya sana mumewe ndiyo kwanza amehamishiwa Geita na alikuwa akaripoti halafu aje kuchukua familia yake,” alisema Ndemanga.


Mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, alisema hadi sasa haijafahamika nini kilitokea na kwamba hilo ni moja kati ya mambo ambayo polisi inachunguza.


“Hayo yote kwamba ilikuwaje akawa chumbani kwa huyo kijana, nini sababu za kifo yatajulikana kadiri upelelezi unavyoendelea,” alisema.


Imeelezwa kuwa jana ilikuwa siku ya askari huyo kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi.


“Mpaka sasa hivi haijajulikana nini hasa kilitokea huko chumbani na ilikuwaje akawa chumbani kwa huyo dereva,” alisema mmoja wa watu waliokuwapo katika eneo la tukio ambaye hata hivyo, hakutaka kutaja jina lake na kuongeza kuwa jana saa sita mchana, mwili wa mwanamke huyo ulichukuliwa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mwanga na kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa uchunguzi.


Taarifa za awali zinasema kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na mikwaruzo shingoni hali inayotia shaka kuwa huenda alinyongwa.


Habari nyingine zinadai kuwa siku ya tukio, mwanamke huyo alikuwa ameaga kuwa anakwenda kanisani lakini baadaye simu yake ilipopigwa ilikuwa ikipokewa na mwanamume.


Ilidaiwa kuwa mume wa marehemu alipojaribu kupiga simu ya mkewe, ilikuwa ikipokelewa na mtu aliyeonekana kuwa ni mlevi wa kupindukia hali iliyomtia wasiwasi na kuamua kuwapigia simu marafiki zake wa karibu ili wamsaidie kumtafuta ndipo walipopata taarifa kuwa ulikuwapo uhusiano kati ya shemeji yao na dereva huyo wa bodaboda.


Ilidaiwa kuwa marafiki hao walikwenda moja kwa moja nyumbani kwa dereva huyo wa bodaboda ambako walimkuta akiwa amelewa na walipoingia ndani walimkuta shemeji yao akiwa ameshafariki dunia.”Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa alikuwa kwenye ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda huko Gonja wilayani Same.MWANANCHI

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI