RAIS KIKWETE AMWAMBIA JANUARI MAKAMBA KUWA ANAPENDA MAMBO MAKUBWA, NI YA KUWANIA URAIS 2015 NDANI YA CCM.

Mbunge huyo wa Bumbuli, ambaye ni mtoto wa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba, alitangaza uamuzi huo akiwa Uingereza alikokuwa akihudhuria mkutano wa sekta ya mawasiliano baada ya kuhojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na baadaye kufafanua nia hiyo katika mahojiano na gazeti hili.
Tanga.
 

Rais Jakaya Kikwete amezungumzia nia ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba kutaka kuwania urais mwakani, akisema mwanasiasa huyo kijana “anataka mambo makubwa, lakini hajamshirikisha”.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kutoa maoni yake kuhusu wanachama wa CCM wanaotaka kuwania urais, baada ya chama hicho kuwaonya makada sita kwa tuhuma za kuanza mapema kampeni za kutaka nafasi hiyo kubwa.


Akiwa jijini London, Makamba alitangaza nia yake ya kuwania urais mwaka 2015, akisema huu ni wakati wa fikra mpya ambazo zinahitaji vijana na kwamba wazee wakae kando.


Jana, Rais Kikwete, ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Soni Bumbuli mkoani Tanga anakoendelea na ziara ya siku tano, alimtaka Makamba “asilazimishe” kwa kuwa wakati ukifika atapata kile anachokitaka.


“Nasikia kuwa bwana mdogo January anataka mambo makubwa. Mie hajaniambia, na mie nasikia. Hata alipogombea ubunge hakuniambia nilisikia baadaye... asilazimishe, wakati ukifika atapata, na akikosa asilete nongwa,” alisema Rais Kikwete.


Rais Kikwete alitoa mfano wake mwenyewe aliposhindwa katika uteuzi wa mgombea urais wa CCM mwaka 1995, wakati akiwa na miaka 45 (miaka minne zaidi ya umri wa Makamba ifikapo 2015), akisema kuwa hakukata tamaa na aliendelea kusikiliza ushauri wa wazee hadi alipofanikiwa kukalia nafasi hiyo ya juu mwaka 2005.


Mwenyekiti huyo wa CCM, ambaye pia ushawishi wake unaweza kuamua mteule wa chama, alimtaka mbunge huyo wa Bumbuli asikilize ushauri wa wazee.


Pamoja na ushauri huo kwa mwandishi wake wa zamani wa hotuba, Rais Kikwete alimpongeza kwa kazi nzuri ya ubunge jimboni humo na akaeleza kuwa anamsaidia katika wizara yake.


Alinukuu maneno ya aliyekuwa katibu mkuu wa Afro Shiraz na swahiba wake, Thabit Kombo aliyemwambia Kikwete kuwa “wakati ukifika utapata”, hasa kutokana na kiu yake ya muda mrefu ya kuwatumikia Watanzania.


“Nilipokosa mwaka 1995 sikukata tamaa, ndipo 2005 nikaingia, na huo ndio ulikuwa wakati wangu wa kushika wadhifa huu. Wakati ukifika watu watake wasitake utakuwa wewe tu,” alisema Kikwete.


Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja takriban wiki moja baada ya Makamba kueleza nia yake ya kuwania urais akisema kwa asilimia 90 ameshaamua kuingia katika kinyang’anyiro hicho.


Mbunge huyo wa Bumbuli, ambaye ni mtoto wa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba, alitangaza uamuzi huo akiwa Uingereza alikokuwa akihudhuria mkutano wa sekta ya mawasiliano baada ya kuhojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na baadaye kufafanua nia hiyo katika mahojiano na gazeti hili.


Rais Kikwete akimshauri asikilize ushauri wa wazee, wakati akitangaza nia hiyo Makamba alisema: “Ni wakati wa fikra mpya kushika dola na mimi ninaona kwamba wazee wakae kando. Mfano awamu moja inapoondoka na wazee walioko katika mfumo wakae kando ili kupisha fikra mpya kuongoza dola.” alisema Makamba ambaye kwa sasa ana miaka 40.


Makamba ameendelea kusisitiza nia yake hiyo na kutetea nafasi ya vijana katika nafasi hiyo kwenye ukurasa wake wa facebook akisema: “Tanzania mpya inahitaji viongozi wapya, mazoea mapya, fikra mpya na maarifa mapya. Inahitaji kuthubutu mambo makubwa siyo kulinda uzoefu wa nyuma.”


Makamba ni mmoja wa makada sita wa CCM walioonywa na chama hicho mapema mwaka huu kwa kutuhumiwa kuanza mapema kampeni za urais kinyume na utaratibu, lakini chama hicho hakijaona kasoro katika uamuzi wake wa kutangaza nia.


CCM yambariki
Katika hatua nyingine, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimebariki mbio za Makamba baada ya jana kueleza kuwa hajafanya kosa lolote kwa kutangaza nia yake.


Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema alichofanya Makamba ni tofauti na adhabu ambayo chama hicho kilimpa yeye na wenzake watano miezi mitano iliyopita.


Nape aliwataka wanaohoji suala hilo kurejea adhabu iliyotolewa na CCM, Februari 18, mwaka huu kwa makada wake sita baada ya kukutwa na makosa ya kuanza mapema kampeni za urais mwaka 2015, akiwamo Makamba.


Wengine waliokutwa na rungu hilo ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe na William Ngeleja.


“Hili jambo linakuzwa tu wakati katika barua tulizowapa tulieleza wazi. Waambie wawaonyeshe barua ambazo chama kimewapa ili mjue nini ambacho hawatakiwi kukifanya,”alisema Nape.


“Yeye amesema akipewa ridhaa ya kugombea urais, jambo hili halipo kati ya makosa ambayo yalisababisha yeye na wenzake kupewa adhabu.”


Februari 18, mwaka huu Kamati Kuu ya CCM ilitoa adhabu kwa makada hao baada ya kuthibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati kinyume na kanuni za uongozi na uaadili za chama hicho.


Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula aliwahi kukemea tabia ya baadhi ya wana-CCM kutangaza mapema nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao, akisema ni wasaliti wakubwa ndani ya chama.


CCM pia ilitoa mwongozo na kanuni za uchaguzi ambazo Ibara 6 (2) (1-5) ya Maadili ya Viongozi wa CCM inawazuia wanachama kutoa michango, misaada, zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na kufanya kampeni bila ya kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya eneo husika.


Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i), ni kinyume kwa wanachama wake kutafuta kuteuliwa kuwania urais kabla ya wakati.MWANANCHI

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI