TAASISI MBILI ZA SERIKALI ZAWACHUNGUZA KWA KINA WALIOLIPULIWA NA BOMU ARUSHA.

http://www.thehabari.com/wp-content/uploads/2014/04/Mkurugenzi-Mkuu-Idara-ya-Habari-Maelezo-Asa-Mwambene.jpg

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene  


MAJERUHI wa bomu lililolipuliwa katika mgahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine jijini Arusha juzi, wanachunguzwa na Jeshi la Polisi na Idara ya Uhamiaji.



Taarifa za awali ambazo gazeti hili lilizipata jana, zilidai tukio hilo la bomu linatokana ugomvi wa kibiashara. Taarifa hizo zilidai kuwa Jeshi la Polisi lilikuwa linaendesha uchunguzi wa tukio hilo na pamoja na madai kuwa linatokana na ugomvi wa kibiashara.

Alipohojiwa kwa njia ya simu jana juu ya tukio hilo na madai kuwa kuna hisia linatokana na ugomvi wa kibiashara, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene alisema, “ni kweli na mimi nimesikia taarifa hizo, lakini tuviachie vyombo vya ulinzi na usalama, vilifanyie kazi tukio hilo na vitatoa taarifa kamili vikimaliza uchunguzi wao”.

Kwa upande wake, Kamanda wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Daniel Namomba, alisema jana ofisi yake inafanya uchunguzi kuhusu majeruhi wa tukio hilo, kubaini kama uwepo wao nchini ulikuwa ni wa kihalali.

Namomba alisema wanapitia nyaraka zote za majeruhi hao ili kujua kama wapo, waliokuwa wanafanya kazi hapa nchini kwa vibali maalumu; na endapo kulikuwa na watalii kati yao, ambao waliingia nchini kihalali.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, ofisa huyo alisema, “Siwezi kuthibitisha kama majeruhi hao walikuwa hapa nchini kihalali au la, naomba unipe muda kwa kuwa suala hili ofisi yangu inalifanyia kazi na baada ya uchunguzi kukamilika nitatoa taarifa rasmi”.

Kumekuwepo taarifa jijini hapa kwamba mfanyabiashara mwenye asili ya Asia (jina tunalo), ndiye aliyekuwa mwenyeji wa majeruhi hao, wanaodaiwa kuwa watalii, huku taarifa nyingine zikidai ni wafanyabiashara wa madini.

“Majeruhi hawa wapo ambao ni wafanyakazi hapa (Arusha) kwa zaidi ya miaka 15, lakini baadhi yao siyo raia na inadaiwa kuwa ni watalii na wengine wanadai walikuja hapa zaidi ya wiki moja iliyopita kwa lengo la kufanya biashara ya madini,” alisema mmoja wa watu, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Waziri hospitalini.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Seif Rashid alitembelea majeruhi jana katika Hospitali ya Rufaa ya Seliani.

Waziri huyo alilaani vikali kitendo hicho kilichofanywa na watu ambao wanahatarisha amani ya jiji la Arusha, ambalo ni kitovu cha utalii nchini.

Alisema hali za majeruhi zinaendelea vizuri. Alisisitiza kwamba vyombo vya ulinzi na usalama, vinaendelea na uchunguzi kubaini watuhumiwa hao hatimaye wafikishwe kwenye mkono wa sheria.

Matibabu Nairobi.
Waziri alisema endapo wagonjwa watasafirishwa nje ya nchi, serikali haitahusika katika matibabu yao, kwa kuwa anaamini nchini kuna hospitali zenye uwezo mkubwa wa kutibu majeruhi.

Akizungumzia hali za majeruhi hao, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Seliani, Dk Mark Jacobson ambaye ni raia wa Marekani, alisema hali za wagonjwa zinaendelea vizuri.

Lakini, alisema mmoja kati ya wagonjwa hao, ambaye ni mtoto wa miaka (13), Ritwik Khaalelwa, amepelekwa Nairobi kwa matibabu kutokana na hali yake kutoridhisha.

Aidha, alisema Deeptak Gupta aliyepoteza mguu wa kushoto, bado yuko katika chumba cha uangalizi maalumu, kutokana na maumivu makali aliyo nayo na familia yake inafanya utaratibu wa kumhamishia Nairobi kwa matibau zaidi.

Jacobson alisema wagonjwa wengine wawili wanaendelea na matibabu hospitalini hapo. Alisema watatu wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya majeraha waliyoyapata, kuendelea vizuri.

Mbatia ahofu.
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia ametaka Serikali kupitia Idara yake ya Ulinzi na Usalama wa Taifa, kurudi kazini na kufanya uchunguzi wa kina juu ya milipuko ya mabomu, yanayotokea Jijini Arusha na kutoa majibu sahihi ya matukio hayo.

Mbatia, ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa, alisema hayo jana jijini hapa, alipozungumza na waandishi wa habari.

Alisema mashambulio hayo katika jiji la Arusha lenye vivuto vingi vya utalii, yanatisha na yanasikitisha na uchumi wa nchi unaweza kuyumba kwa matukio hayo.

Mbatia alisema Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa kuwa na vivutio vya utalii vingi na uchumi wa nchi katika sekta ya utalii, pato lake ni sawa na asilimia 17 sawa na Sh trilioni 9.6 kwa mwaka.

Alisema watu na mali zao katika maeneo ya Jiji la Arusha na Zanzibar, wanapaswa kulindwa kwa nguvu zote.Alisema serikali inapaswa kufuatilia na kutambua adui wanayepambana naye.

Alishauri serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama, kukusanya kila kiashiria cha matukio hayo bila kudharau na kisha kukaa mezani kwa kushirikisha watu mbalimbali, kuchambua kwa kina kila kimoja kupata ukweli na kisha kuufanyia kazi.

Viashiria.
Alitaja baadhi ya viashiria vilivyowahi kutajwa na makundi mbalimbali kuwa ni ugomvi wa kisiasa, dini, wivu wa kibiashara ya utalii na kusherehekea na kushabikia matukio ya uvunjifu wa amani katika nchi jirani.

Vingine ni ugomvi wa marais na mgogoro wa kutaka kumng’oa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki. Alisema utaratibu wa sasa wa serikali na vyombo vya usalama, kutoa majibu mepesi kila tukio linapotokea, bila kutoa majawabu sahihi, ni dalili za kushindwa kutafutia ufumbuzi matukio hayo, hali inayoendelea kujenga hofu miongoni mwa wananchi.

Alionya kuwa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama, haipaswi kusubiri hadi jambo litokee, ndipo ianze kupambana bali inapaswa kujipanga, ikizingatiwa tukio hilo la jana si la kwanza, bali ni la sita ndani ya kipindi cha mwaka na nusu.

Mbatia alisema alitegemea muda huu angeona anga la Arusha likiwa limefunikwa na helikopta na pia kukiwa na askari wa kutuliza ghasia mitaani.

Alisema kwa mkoa wa Arusha kuendelea kukumbwa na matukio hayo ya mabomu, kunaathiri mambo mengi, ikiwemo pato la taifa, ikizingatiwa utalii unachangia asilimia 33 ya pato la taifa.HABARILEO.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*