Ofisi ya Bunge yatoa ufafanuzi kuhusu malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.

Mkurugenzi wa Habari na Itifaki, Bw. Jossey Mwakasyuka (kushoto) akitoa ufafanuzi mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba leo katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Bunge mjini Dodoma.

Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo wakisikiliza kjwa makini maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Habari na Itifaki, Bw. Jossey Mwakasyuka wakati alipofanya mkutano na waandishi hao kwa lengo la kutolea ufafanuzi kuhusiana na malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba leo katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Bunge mjini Dodoma.
OFISI ya Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, imetoa ufafanuzi juu ya taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari kuhusu kuchelewa kwa malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.

Ufafanuzi huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa Habari na Itifaki Bw. Jossey Mwakasiyuka wakati alopokutana na waandishi wa habari kwa lengo la kutolea ufafanuzi kuhusiana na taarifa hizo zilizoikera ofisi hiyo ya Bunge Maalum.

Mwakasyuka amevieleza vyombo vya habari kuwa, ofisi ya Bunge Maalum imekerwa na kuchapishwa kwa taarifa hizo na baadhi ya vyombo vya habari kwani taarifa hizo ni za upotoshaji na zina lengo la kuwadhalilisha Waheshimiwa Wajumbe na kuwafanya waonekane wenye kuishi na kufanya kazi kwa kutegemea posho wanazolipwa.

“Ni vema ikaeleweka kwamba Wajumbe wa Bunge Maalum wote ni watu wenye nafasi zao katika jamii na ni wenye kazi au shughuli zao mahususi zinazowaingizia kipato na kwamba Ujumbe wa Bunge Maalum ni nafasi ya muda tu ya kutimiza jukumu la kuliandalia taifa Katiba Mpya”. Alisema Mwakasyuka.

Mwakasyuka ameongeza kuwa, si vema kwa vyombo vya habari kuwadhalilisha Wajumbe hao kwa njia yoyote ile kwani kwa kufanya hivyo kunawavunja moyo na kuwafanya washindwe kuifanya kazi ya Bunge Maalum vizuri kama ilivyotarajiwa na wananchi.

Akifafanua kuhusiana na malipo ya posho hizo, Mkurugenzi Mwakasyuka ameviambia vyombo vya habari kuwa, Wajumbe wote wa Bunge Maalum ambao wanahudhuria vikao vinavyoendelea wamekwishalipwa posho zao zote kama wanavyostahili.

“Ni vyema ikaeleweka kwamba malipo ya posho yanafuata taratibu za fedha za umma na yanapita kwenye mchakato maalum unaojumuisha kupata orodha za mahudhurio ya Wajumbe kwenye kikao, upatikanaji wa fedha toka Hazina, na upatikanaji wa fedha toka Benki, hivyo wakati mwingine huchukua siku kadhaa hadi kukamilika.” Alifafanua Mwakasyuka.

Aidha, Mwakasyuka amevitahadharisha vyombo vya habari  vinavyondika habari za Bunge Maalum kuzingatia maadili na kanuni za Uandishi wa habari zinazotolewa katika vikao vya Bunge Maalum ili taarifa kama hizo za upotoshaji zisijirudie tena.

“Kumbukeni kuwa wajibu wenu ni kuhabarisha umma na sio kupotosha umma na hata kuleta usumbufu kwa jamii kutokana na uandishi usio makini”. Alionya Mwakasyuka.

Katika kanuni za Bunge Maalum, kanuni ya 77 inawataka waaandishi wa habari kuandika habari za Bunge Maalum kwa weledi mkubwa kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa Habari ili kuondoa uandishi wenye kuleta chuki kati ya Serikali na Wananchi wake kwani kinyume na kanuni hiyo, Katibu anaweza wakati wowote kuondoa ruhusa aliyotoa kwa mwakilishi wa chombo chochote cha habari iwapo chombo hicho kitatoa taarifa yoyote kuhusu shughuli za Bunge Maalum ambayo kwa maoni ya Bunge Maalum inapotosha ukweli au vinginevyo inakiuka kanuni, taratibu au haki za Bunge Maalum.
na fredy mgunda

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU