WAKATI baadhi ya
wanaharakati wakishinikiza Bunge Maalumu la Katiba liahirishwe Mwenyekiti wake,
Samuel Sitta (pichani) amesema kamwe halitavunjwa ili kuokoa fedha za wananchi
zilizotumika.
Kutokana na hilo
alisema kuwa kuahirishwa kwa Bunge hilo, hatua ambayo hata hivyo pamoja na kuwa
kumekuwepo na shinikizo kubwa kutaka hatua hiyo ichukuliwe, haitawezekana kwa
mujibu wa sheria.
Sitta alisema hayo
jana ofisini kwake bungeni mjini hapa wakati alipokutana na ujumbe kutoka Mfuko
wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) ulioambatana na baadhi ya wanahbari wa vyombo
mbalimbali.
Alisema anashangaa
wanaoshinikiza liahirishwe jambo ambalo litakuwa ni sawa na kuteketeza fedha za
wananchi kwa vile mchakato ulianza muda mrefu zaidi ikilinganishwa na muda
uliobaki.
Sitta ambaye pia
ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki alisema vikao vya Bunge hilo
vinaendelea kufanyika kihalali kama sheria inavyobainisha na kuwa lingeweza
kusitishwa kama wajumbe wa kundi moja wangetoka wote.
Alisema kuwa
makundi yote yote yapo na yanahudhuria vikao vya kamati yakiwemo Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kundi la 201 huku akisisitiza kuwa yeye anaaamini
Katiba itakayopatikana itakuwa bora.
Mwenyekiti huyo, alionesha
kutoridhishwa na kutokuwepo kwa uwazi katika uendeshaji wa Serikali, hali ambayo
inasababisha wanahabari hapa nchini kupata wakati mgumu katika utendaji wao.
Kwa upande
mwingine alisema wamepokea mapendekezo ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuhusu
Baraza la Habari kuingizwa katika Rasimu ambayo inaendelea kujadiliwa na
wajumbe kupitia kamati zao.
Wakati hayo
yakijiri, wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakikosekana
katika kamati mbalimbali kwenye Bunge la Katiba linaloendelea, Mwenyekiti wa
Kamati namba 8, Job Nduga amesema akidi inatosha.
Alisema katika
kamati yake Mjumbe, John Shibuda ambaye ni miongoni mwa wajumbe sita wa Ukawa
anaendelea kushirikiana na kamati hiyo yenye jumla ya wajumbe 52 inayokutana
kupitia sura mbalimbali za Rasimu.
Ndugai ambaye pia
ni Naibu Spika alibainisha kuwa wajumbe wenzake wanaendelea na majadiliano kwa
maelewano na wameweza kupiga kura kwa utaratibu mzuri ingaa kumekuwa na
mgongano wa hoja.
Suala la uraia wa
nchi mbili yaani uraia pacha kwa mara nyingine limetikitisa Bunge Maalumu
hususan katika kamati hiyo namba 8 huku wanaopendekeza suala hilo wakishutumiwa
kwa kukosa uzalendo.
Comments