Ndege ya Kampuni ya Safari Express Limited imeanguka katika
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuwateketeza watu watatu waliokuwamo
ndani.
Ndege hiyo yenye namba za usajili 5Y-SXP iliruka
kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza Jumapili saa 1:26 usiku ikielekea
Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) Kenya ambako ilitakiwa kutua saa
2:36 usiku.
Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa
(Tanapa), Paschal Shelutete alikiri ndege hiyo kuanguka kwenye hifadhi
hiyo na walikuwa katika harakati za kuitafuta.
Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege nchini, kutoka
Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, David Nyamwihura alisema ajali hiyo
ilitokea takriban maili 20 kutoka Serengeti, katika eneo la Kogatembe na
watu wote watatu waliokuwamo wamefariki dunia.
Meneja wa Udhibiti wa JKIA, Clever Davor
aliliambia gazeti la Daily Nation la Kenya kuwa ndege hiyo ilipoteza
mawasiliano na rada ya uwanja huo ikiwa imeruka angani urefu wa futi
14,000.
Awali, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KCAA)
ilitoa taarifa juu ya kuchelewa kwa ndege hiyo iliyokuwa ikitarajiwa
kutua katika uwanja wa JKIA saa 2 usiku.
Jana asubuhi, Kamanda wa Viwanja vya Ndege wa Kenya (KAPU),
Joseph Ole Tito alithibitisha kupotea kwa ndege hiyo kabla ya kuonekana
baadaye katika Hifadhi ya Serengeti.
Polisi wa Kenya hawakueleza ndege hiyo ya mizigo aina ya Fokker F-27-500 ilikuja nchini kwa shughuli gani.
Ndege zote zinazotoka Kenya kwenda nchi za jirani,
huanzia safari zake katika viwanja vya JKIA, Wilson au Wajir ili kuwa
na usimamizi wa karibu.
Watano wafa ajalini Moro
Katika hatua nyingine, watu watano wamefariki
dunia papo hapo na mmoja kujeruhiwa baada ya gari dogo walilokuwa
wakisafiria kwenda kwenye sherehe kugongana uso kwa uso na lori.
Ajali hiyo ilitokea Jumamosi iliyopita saa 2:30
usiku eneo la Hoteli ya Tabu, Wilaya ya Gairo na kuhusisha gari dogo
aina ya Toyota Corola lililokuwa likiendeshwa na Joashi Mrisho (25) na
lori lililokuwa likienda Burundi.
Comments