KINANA ATAKA AJIRA YA UTUMISHI SASA IWE MIAKA MITATU

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akihutubia katika mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Tangamano, jijini Tanga, wakati akihitimisha ziara ya siku 11 katika wilaya zote za Mkoa wa Tanga. PICHA NA RICHARD MWAIKENDA;KAMANDA WA MATUKIO BLOG

Na Mwandishi Wetu, Tanga.

SERIKALI imetakiwa kutimiza wajibu wake wa kuwatumikia Watanzania na si kuendelea kutoa ahadi na mipango isiyotekelezeka na kugeuka kuwa hadithi.

Wakati kwa mkoa wa Tanga, Serikali imetakiwa kujenga reli ya kisasa na bandari katika mkoa huo na si kila siku kuwaaambia wananchi kuwa mchakato unaendelea wakati hakuna kinachofanyika.

Pamoja na hayo, ni vema Serikali ikaangalia upya mfumo wake wa ajira na anapendekeza ajira ya utumishi wa umma iwe ya miaka mitatu badala ya miaka 60 ambayo inasababisha watumishi kushindwa kutimiza majukumu yao.

Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrhaman Kinana wakati akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Tanga ikiwa ni hitimisho la ziara yake kwa mkoa huo ambapo amekutana na wananchi na kusikiliza kero zao.

Kinana katika mkoa huo amefanya mikutano ya hadhara  76, amekagua miradi ya maendeleo 72 na jumla ya mzunguko wake Tanga ametembea kilometa zaidi ya 3000.

Akizungumzia kuhusu utendaji wa Serikali, Kinana alisema  watendaji wengi wao wamekuwa na kiburi kwa wananchi na wameshindwa kutimiza wajibu wao kwa umma lakini wamekuwa wakipokea mishahara na mambo yao yamenyooka wakati wananchi wako hoi bin taaban.

"Watendaji wengi wa Serikali wamekuwa kiburi kwa wananchi.Wamekuwa na uhakika na ajira zao maana watalipwa mishara hadi miaka 60, matokeo yake hakuna ambacho wanakifanya.

"Wameamua kujilinda kwa kuwa na sheria ya utumishi wa umma ambayo hakuna mahali inasema mtumishi akikosea afukuzwe kazi.Sheria hiyo imekaa ya kulindana tu.

"Ndio maana mtumishi wa umma anaharibu kazi mahali fulani na baada ya hapo anahamishiwa sehemu nyingine.Wapo wengine wanaharibu lakini badala ya kufukuzwa wanapandishwa vyeu huku wakiendelea kulipwa mishahara na kutumia magari ya Serikali,"alisema Kinana.

Alifafanua mfumo wa watendaji wa Serikali kutochukuliwa hatua, ndio umesababisha kwa sehemu kubwa wananchi kukosa huduma zinazotakiwa kutolewa na watendaji hao ,hivyo muda wa kulinda umefika mwisho.

"Hakuna sababu ya kulinda, wanaoharibu kazi na kushindwa kutimiza wajibu wao lazima wawajibishwe.Tena ikiwezekana mfumo wa ajira ubadilishwe badala ya mtumishi kukaa miaka 60, awe na mkataba wa miaka mitatu , mitatu.

"Hii itasaidia pale ambapo mtumishi ameshindwa kufanya kazi badala kukaa hadi afikishe miaka 60 astaafu basi atimuliwe ili wenye uwezo wa kufanya kazi wapewe nafasi ya kuwatumikia Watanzania.Tukiwa na mfumo wa ajira ya mkataba wa miaka mitatu watumishi na watendaji watafanyakazi kwa bidii,"alisema Kinana.

Kuhusu ahadi na mipango inayotolewa na Serikali, alisema ufike wakati badala ya kila siku waanchi kuwaambia mchakato unaendelea, au Serikali iko mbioni ifike mwisho maana wananchi wamechoka kusikia, wanataka kuona utekelezaji.

"Wananchi wanahitaji kuona utekelezaji, hakuna sababu ya kila siku kuambiwa mchakato unaendelea, wako mbioni na mbio zenyewe hazishi.

"Tunaomba tuseme wazi Serikali ya CCM nasi tunakila sababu ya kukiri udhaifu lakini tunaomba wananchi mtuamini.Tutahakikisha tunashikana mashati ili tutwatumikie kwa uadilifu mkubwa,"alisema Kinana.

Akizungumzia uchumi wa mkoa wa Tanga, alisema njia pekee ya kuinua uchumi wa mkoa huo ni kujengwa kwa bandari na uboreshwaji wa reli ya mkoa huo na si kingine lakini kwa bahati mbaya imekuwa hadithi maana kila siku inaelezwa mipango ambayo imeshindwa kutekelezwa.

Alisema anakumbuka Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi akiwa madarakani, alifanya mazungumzo na Rais Yower Museven wa Uganda kwa ajili ya ujenzi wa reli ya Tanga lakini hadi leo hii hakuna ambacho kimefanyika na kila kiongozi anazungumzia mipango ambayo kimsingi imekuwa hadithi.

Alisema wananchi wa Tanga sasa wanataka kuona reli inajengwa na bandari inajengwa, mambo ya kila siku kuwaeleza mipango na ahadi inatosha maana inawaumiza vichwa tu na dawa zenyewe hakuna.

Aliwahakikisha CCM itatoka na majibu kuhusu ujenzi wa reli na bandari kwa mkoa huo wa Tanga ambayo ndiyo yenye kuinua uchumi wa wananchi hasa kwa kuzingatia kuna kundi kubwa la vijana halina ajira.

"Wananchi hawa wa Tanga wanachotaka kuona ujenzi wa bandari unaaanza, au reli imeanza kuboreshwa,hawataki kusikia kuhusu mipango inayotolewa na Serikali kuhusu uboreshwa wa reli na bandari.

"CCM tutakuwa na Kamati Kuu(CC), mwezi huu, moja ya mambo ambayo tutayazungumza na kutafuta ufumbuzi wake ni hili la bandari na reli ya Tanga.Ifike mahali wananchi waone utekelezaji maana ndio uchumi wao, ndio maisha yao,"alisema Kinana.

Wakati kwa upande wa mbunge wa Tanga Mjini Omar Nundu, alisema kuwa watendaji wengi wa Serikali wamekuwa wakikwamisha utekeleza wa maendeleo ya wananchi na hiyo inatokana na ukweli wa kwamba hawana moyo wa CCM.

"kuna tatizo kwa baadhi ya watendaji wa serikali, wamekuwa wakikwamisha maendeleo, nakumbuka nikiwa waziri, nilijifunza mengi, maana pale wizarani ukiondoa waziri, naibu waziri , watendaji waliobaki wengi wao hawana moyo wa kutekeleza miradi ya maendeleo.

"Pamoja na hayo serikali ya ccm imefanya mambo makubwa kwa ajili ya wananchi na kwa mkoa wa tanga kuna mengi yamefanyika ya maendeleo.kupitia mfuko wa jimbo tumefanya maendeleo makubwa.


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA