WATOTO 130000 WANAISHI NA VIRUSI VYA UKIMWI

      

unnamed
Wajumbe kutoka asasi za umma na za binafsi za ndani na nje ya nchi zinazoshughulikia mambo ya Ukimwi waliohudhuria kongamano la nne la kitaifa linalohusu Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi kwa watoto wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa ufunguzi wa kongamano hilo. Hadi sasa watoto wenye maambukizi ya VVU 130000 wameweza kufikiwa kati ya hao 39317 wamepewa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo.
Picha na Anna Nkinda – Maelezo
unnamed1
Baadhi ya wajumbe kutoka asasi za umma na za binafsi za ndani na nje ya nchi zinazoshughulikia mambo ya Ukimwi wakimsikiliza Naibu waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt. Pindi Chana (hayupo pichani) wakati akifungua kongamano la nne la kitaifa linalohusu Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi kwa watoto. Kongamano hilo la siku mbili limeandaliwa na Taasisi ya Elizabeth Glaser Pediatric Aids (EGPAF).
……………………………………………………………………………..
 TAKWIMU zinaonesha kwamba watoto 130000 wana maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) kati ya hao 39317 wamefikiwa na kupatiwa huduma ya dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt. Pindi Chana wakati akifungua kongamano la nne la kitaifa la VVU na UKIMWI kwa watoto linalofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere uliopo jijini Dar-es-salaam.
Dkt . Chana alisema asilimia 39 ya watoto walio katika hatari ya kupata maambukii ya UKIMWI hupimwa vipimo vya kubaini maambukizi ya VVU ndani ya miezi miwili baada ya kuzaliwa hivyo basi kuna umuhimu kwa watoto hawa kupata huduma za tiba mapema.
Akizungumzia maambukizo ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto waziri huyo alisema Tanzania imepiga hatua katika kuzuia maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto lengo likiwa ni kutokomeza kabisa maambukizi mapya kwa watoto wachanga.
“Mama wajawazito na wale wanaonyoyesha wanapatiwa huduma ya dawa za kupunguza makali ya VVU mara tu wanapogundulika kuwa na maambukizo, kupitia mpango mpya unaojulikana kama ‘uwezekano namba 2 au (Option B+)”, alisema Dkt.Chana
Alisema kufikia mwezi Juni mwaka huu jumla ya akina mama 940900 kati ya 1050043 hii ni sawa na asilimia 89.6% ya waliohudhuria kliniki walipimwa UKIMWI kati ya hao 47856 takribani asilimia 5 walikutwa na maambukizi ya VVU.
Kwa upande wa watoto 20569 walipima kipimo cha DBS kati ya hao 2063 hii ni sawa na asilimia 10 walikutwa na maambukizo ya VVU.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Donan Mbando, alisema ingawa nchi imepiga hatua katika mapambano ya kudhibiti UKIMWI hali halisi inaonyesha kuwa bado kuna maambukizo yanatokea sio tu kwa watu wazima bali na kwa watoto pia.
“Ni jukumu letu kuendelea kuweka mikakati ya dhati na kuisimamia ili kuhakikisha lengo la kutokomeza maambukizo ya VVU tunalifikia kwani mwaka 1986 maambukizi yalikuwa juu kwa asailimia 18 lakini hivi sasa yameshuka na kufikia asilimia 5.3”, alisema Dkt. Mbando
Kwa upande wake Mkurugenzi wa ufundi kutoka Taasisi ya Elizabeth Glaser Pediatric Aids (EGPAF) ambao ni waandaaji wa kongamano hilo Chrispin Kimario alisema ni muhimu kwa wazazi na jamii kushirikiana kwa pamoja na kulibeba jukumu la kuhakikisha kila mama mjamzito anapata huduma ya vipimo husika na matibabu kwa wakati.
Kimario alisema, “Watoto wameachwa nyuma, ni vyema tukumbuke kuwa mtoto hawawezi kujipeleka wenyewe hospitali kupima afya zao, hivyo ni jukumu letu wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto hawa wanapata huduma wanazostahili”.
Kauli mbiu ya kongamano hilo la siku mbili ambalo limehudhuriwa na wadau wa afya kutoka asasi za umma na binafsi za ndani na nje ya nchi ni ongeza kasi: Rahisisha upatikanaji wa utumiaji wa huduma za VVU na Ukimwi, pata matokeo chanya ya afya za mama na watoto wanaoishi na VVU.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA