MAMA KIKWETE AWATAKA WAKAZI WA WILAYA YA LINDI MJINI KUHAKIKISHA WATOTO WAO WANAKWENDA SHULE

 PICHA NA JOHN LUKUWI
……………………………………………………………………………………..
Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
13/12/2014 Wakazi wa wilaya ya Lindi mjini wametakiwa kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule na kusoma kwa bidii kwani Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imejenga shule za kutosha  katika kata zote za wilaya hiyo.
Mwito huo umetolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwa nyakati tofauti na wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni ya uchaguzi wa Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za mitaa uliofanyika katika Kata za Chikonji na Mingoyo.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema wakati ujenzi wa shule hizo unaanza vyama vya upinzani walizidharau na waliziita za yeboyebu kwa lengo la kuwakatisha tamaa lakini Serikali ya CCM kwa kushirikiana na wananchi hawakukata tamaa na kuendelea na ujenzi.
“Zamani wanafunzi waliokuwa wanajiunga na elimu ya Sekondari walikuwa wachache baada ya kukamilika kwa ujenzi wa shule hizi hivi sasa kila mwanafunzi anayefaulu mtihani wa darasa la saba anajiunga na elimu ya Sekondari haya ndiyo maendeleo yaliyoletwa na CCM”.
Ili uweze kuendelea ni lazima ukutane na changamoto nasi katika shule hizi tulikutana na changamoto za walimu na maabara, vyuo mbalimbali nchini viliweza kutoa walimu wengi  na kupunguza tatizo la walimu wa masomo ya sanaa na miaka michache ijayo watapatikana walimu wa kutosha wa masomo ya sayansi”, alisema Mama Kikwete.
Aliendelea kusema wakati wa ujenzi wa shule za Sekondari za Kata kulisahaulika ujenzi wa maabara kwa ajili  ya masomo ya sayansi, hivi sasa Serikali kwa kushirikiana na wananchi wanamalizia kazi ya ujenzi wa  maabara katika shule hizo  na hivyo kuwafanya  watoto kusoma masomo ya sayansi kwa fasaha zaidi.
MNEC huyo pia aliwataka wananchi hao kuchagua viongozi wanaofaa kwani uchaguzi ni kwa ajili ya kutengeneza maisha yao kwa  kipindi cha miaka mitano hivyo basi wasiweke rehani maisha yao kwa kufuata mkumbo na kuchagua viongozi wasiofaa.
Kwa upande wake Katibu wa CCM mkoa wa Lindi Adelina Gefi alisema katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji chama hicho kitapata ushindi wa kishindo kwani hadi hivi sasa ndani ya  mkoa huo wagombea katika vitongoji 600, vijiji 80 na mitaa saba wamepita  bila kupingwa.
Gefi alisema CCM inaleta maendeleo na upinzani unachelewesha hivyo basi siku ya uchaguzi ikifika wananchi wajitokeze kwa wingi na kuwachagua wagombea wa chama hicho ili  wawaletee maendeleo.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya  Chikonji mwanachama mmoja aliyejulikana kwa jina la Abdallah Mohammed Kilimbalimba kutoka Chama cha Wananchi (CUF) alijiunga na Chama Cha Mapinduzi.
Mama Kikwete yupo wilayani humo kwa ajili ya kushiriki  kwenye kampeni na kuwanadi wagombea wa chama hicho wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji  unaotarajiwa kufanyika kesho nchini.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI