SHIRIKA LA BANDARI ZANZIBAR LAZINDUA TAGI MPYA YA KUSAIDIA MELI KUBWA KUINGIA NA KUTOKA GATINI

      

……………………………………………………………………………
Na Miza Kona Na Abdalla Ali – Maelezo Zanzibar
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri amewataka wafanyakazi wa Shirika la Bandari Zanzibar kufanya kazi kwa juhudi na ufanisi kwa lengo la kuleta maendeleo na mabadiliko nchini.
Hayo ameyaeleza huko katika Shirika la Bandari Zanzibar wakati akizindua Tagi mpya ya Shirika hilo MV Shuwari ikiwa ni miongoni mwa  shamrashamra za kusherehekea miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema bandari ni chachu ya maendeleo katika nchi yoyote Duniani na muhimili mkuu wa kuleta maendeleo na mabadiliko yatakayofanywa kwa ufanisi na juhudi kubwa zitakazoweza kuinua uchumi wa  nchi.
Amefahamisha kuwa utendaji wa kazi unategemea rasilimali watu na vifaa vya kisasa vinavyo kwenda sambamba na mazingira ya kazi yatakayoleta maendeleo na mabadiliko ya haraka katika kutoa huduma za utendaji.
“Utendaji wa kazi unategemea rasilimali watu na vifaa vya kutosha na vya kisasa ambavyo vinakwenda sambamba na mazingira ya kazi ambavyo vitaleta maendeleo na mabadiliko ya haraka katika kutoa huduma za utendaji”, Alieleza Waziri Omar.
Aidha Waziri Omar ameeleza kuwa ufinyu wa nafasi ya kuhifadhia mizigo bandarini hapo, pamoja na Wafanyabiashara kutoondosha Makontena yao kwa wakati ndio changamoto kubwa zinazoikabili bandari hiyo.
Waziri Omar pia amewataka wafanyabiashara kuchukua juhudi za kutoa mizigo yao bandarini kwa wakati ili kuondosha msongamano uliopo na kulipa ushuru wa mizigo hiyo ili kuliongezea pato la Taifa.
Amesema madhumuni ya Tag hiyo ni kuimarisha ufungaji na ufunguaji wa meli bandarini hapo hivyo mategemeo makubwa ni kuona kuwa inatumika ipasavyo kwa kufuata ushauri na maelekezo ya wataalamu kwa lengo la kuleta maendeleo ya bandari na taifa kwa ujumla.
Nae Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Cpt. Abdalla Juma Abdalla amesema Tagi Mv Shuwari tayari imeshaanza kazi ya kusaidia kufunga na kufungua meli gatini ambayo inauwezo wa kukabiliana na  majanga ya moto pamoja kusaidia kuokoa maisha ya watu inapotokea ajali ya meli au boti baharini.
Amesema Tagi hiyo imejengwa kwa udhamini wa kampuni ya Damen Shipyards ya Uholanzi kwa kushirikiana na Shirika la Bandari la Zanzibar na imegharimu Tsh.zaidi Bilioni 10 ambapo Bilioni 6.9 ni mkopo kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) na ghrama zilizobaki zimelipwa na Shirika la Bandari.
Tag hiyo ina urefu wa mita 22.64, upana mita 7.84, kina cha kueleya mita 3.50, nguvu zake 2720 HP, mwendo 11.70 knots, nguvu za kuvuta tani 38, na uzito wa tani 140 inatarajia kuleta maendeleo makubwa bandarini hapo.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU