WABUNGE WAPIGANA VIKUMBO NA WATU WANAOWANIA KURITHI MAJIMBO YAO.

 
Shughuli za Bunge zilipokuwa zikiendelea Bunge lililopita, Wabunge wengi wameanza mchakato wa kutaka kurudi tena katika jengo hili huku wengine wapya wakitafuna namna ya kutaka kuingia. Picha na Maktaba.


Dar/Mikoani.
Wakati ikiwa imesalia siku chache kabla ya kipenga cha kuruhusu wananchi kujitokeza kuwania urais, ubunge na udiwani, moto unawaka kwenye majimbo mbalimbali ambako wabunge wanapigana vikumbo na watu wanaoonekana kutaka kuwarithi.



Vita iliyo wazi ni ile inayohusisha wenyeviti wa vyama vya NCCR-Mageuzi na TLP, James Mbatia na Augustine Mrema ambao wameshatoleana maneno ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, lakini mchuano ni mkali kwenye majimbo mengine, wakiongozwa na mbunge wa CCM, Ester Bulaya ambaye ameeleza dhamira yake ya kutaka Jimbo la Bunda, ambalo linashikiliwa na Waziri wa Chakula na Kilimo, Steven Wassira pamoja Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Ummy Mwalimu ambaye ameonyesha nia ya kwenda Tanga.


Mchuano huo unazidishwa na kitendo cha wabunge walioingia kwenye Bunge la Kumi kwa tiketi ya viti maalumu, ambao sasa wataka kurejea kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kwa kuchaguliwa na wananchi.


Wabunge wengi wa viti maalumu wameanza kuonyesha makucha majimboni wakifanya shughuli mbalimbali za kijamii katika kile kinachoonekana ni kujiweka karibu na wananchi. Wengi wanajishughulisha na kuchangia masuala ya maendeleo pia kuendesha au kudhamini mashindano mbalimbali ya mpira wa miguu.


Kwenye baadhi ya majimbo, mchuano ni mkali zaidi kutokana na ukweli kuwa waliokuwa wanayashikilia na ambao baadhi walikuwa wanaonekana mibuyu, kutangaza kutorudi tena kuomba kura kutokana na kuona imetosha au kufikiria kuwania nafasi nyingine.


Muungano wa vyama vya upinzani, Ukawa, pia umeongeza joto hilo kutokana na ukweli kuwa vyama vya NCCR-Mageuzi, NLD, CUF na Chadema vimepania kusimamisha mgombea mmoja kwenye majimbo mengi.


“Nimetafakari kufuatia maelekezo ya chama changu, nimejipima na nimetazama hali halisi ya maendeleo na kero ya huduma na matatizo, nikaona ni wakati wa kutatua haya,” alisema Abdulaziz Ahmad alipoulizwa kuhusu nia yake ya kuwania ubunge wa Jimbo la Lindi, ambalo kwa sasa linashikiliwa na Salum Barwany wa CUF.


Mwanachama mwingine wa CCM, Joseph Mhagama, ambaye analitaka Jimbo la Peramiho linaloshikiliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Utaratibu wa Bunge, Jenister Mhagama, alisema haoni kama mbunge wa sasa anawatumikia wananchi.


“Nalitaka jimbo kwa lengo la kuleta mabadiliko zaidi kwa kuwa mbunge wa sasa siyo mkaaji jimboni,” alisema Mhagama ambaye ni mkurugenzi wa Shirika la Ruccodia.


Hata hivyo wabunge wanaotaka kuendelea wanajitetea kuwa wamefanya mengi na wanataka kuyaendeleza.


“Ninajiona kwa sasa hakuna mtu zaidi yangu,” alisema mbunge wa sasa wa Same Magharibi, Dk David Mathayo David alipoulizwa kuhusu kinyang’anyiro cha ubunge jiomboni kwake.


“Nimefanya mengi na bado nataka kuendelea kufanya mengi zaidi lakini natimiza haki yangu ya kidemokrasia kwamba wakati ukifika wa kugombea, haki inaniruhusu. Na mwisho tumeyaanza mengi na tunataka tuendeleze hayo tuliyoanzisha.”


Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, ambaye ameshaeleza kuwa atarejea kutetea jimbo lake na kutabiri ushindi wa kishondo, alisema jana kuwa ameshatimiza zaidi ya asilimia 90 ya ahadi alizoahidi mwaka 2010 na hadi kufikia Juni atakuwa amefikisha asilimia 100.


“Kwa mazingira yaliyopo, bado wananchi wanamhitaji Sugu na siyo Sugu peke yake, wanapanga mkakati wa kuhakikisha wanaichukua halmashauri ili iwe chini ya Chadema,” alisema mbunge huyo kijana.


Hadi sasa wabunge ambao wameshaweka bayana kutorejea tena majimboni ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambaye ni mbunge wa Mtama, Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutoka Jimbo la Katavi.


Wengine wanaoachia majimbo yao ni Hezekiah Chibulunje (Chilonwa), Deogratius Ntukamazina (Ngara), Spika wa Bunge, Anne Makinda (Njombe Kusini) na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye ameeleza kuwa ameshawatimizia wananchi wa Kigoma Mjini mahitaji yao na sasa anaangalia kwingine.


Pia yumo mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ambaye anatajwa kutaka kuwania urais kwa tiketi ya CCM, ametangaza kutogombea tena ubunge, sambamba na mbunge wa Longido, Lekule Laizer na Mustapher Mkullo.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA