CBE YAWAKUMBUKA WAMACHINGA, YAENDESHA UTAFITI KUWASAIDIA KUTAMBULIWA RASMI.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam  Prof.  Simon Msanjila (kushoto) akitoa ufafanuzi kuhusu  mchango wa utafiti  wa shughuli za wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga) unaofanywa na chuo hicho kwa kushirikiana  na  Shirika la Wafanyabiashara  kutoka nchini  Finland (FBMA) utakavyochangia maendeleo ya sekta ya biashara nchini.


Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) kwa kushirikiana  na  Shirika la Wafanyabiashara  kutoka nchini Finland (FBMA)  kinafanya utafiti  wa wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga) kwa lengo la kubaini  fursa za biashara zilizopo , faida, changamoto  na mchango wao katika maendeleo ya taifa pindi watakapoingizwa kwenye mfumo rasmi unaotambulika kisheria.   

Akizungumzia utafiti huo leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema amesema kuwa kwa kipindi kirefu wafanyabiashara wadogowadogo maarufu kama wamachinga wamekuwa katika malumbano na mamlaka za miji na majiji kote nchini kutokana na kukosa mfumo rasmi unaotambua biashara zao.

Amesema chuo chake kwa kuliona jambo hilo kikishirikiana na Shirika la Wafanyabiashara wa Finland (FBMA) kimeamua kuendesha utafiti huo kuanzia mwaka 2014 na kuongeza  kuwa matokeo ya awali yaliyopatikana ndani ya mwaka mmoja yamebainisha kuwa jiji la Dar es salaam lina wamachinga zaidi ya Laki saba (700,000) wanaofanyabiashara zao nje ya mfumo rasmi unaotambulika kisheria.

“Katika utafiti tumegundua kuwa Dar es salaam ina wamachinga wengi zaidi kuliko maeneo mengine walio nje ya mfumo rasmi unaotambuliwa na Serikali hii ni fursa, kwa sasa hakuna mfumo wowote unaotambua uwepo wao na baadhi yao wamekuwa wakilumbana na vyombo vya usalama na mamlaka husika jambo lililojenga uadui miongoni mwao” Amesema Prof. Mjema.
Amesema katika kutatua changamoto hizo utafiti huo utaangalia jinsi gani wamachinga watatambulika kisheria katika mfumo rasmi , pia kukisaidia Chuo cha Elimu ya Biashara kuandaa mitaala na programu mbalimbali za masomo ya biashara kwa vijana hao ambao wengi wao wameishia elimu ya darasa la 7 ili kuwajenge uwezo wa kutunza kumbukumbu za biashara zao pamoja na kuiwezesha Serikali kuweka utaratibu wa wafanyabiashara hao kufikiwa na huduma muhimu katika maeneo yao.

Aidha, amesema utafiti huo utawasaidia wafanyabiashara hao kuepuka hasara wanayoipata mara kwa mara kutokana na bidhaa zao kukamatwa na wakati mwingine kuharibiwa na mamlaka zinazohusika wakati wa oparesheni mbalimbali za kuwaondoa katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria kufanya biashara.

“Katika utafiti huu tunapendekeza kuanzishwa kwa mfumo rasmi wa kuwatambua  wamachinga wote kote nchini ili waweze kujulikana  na  shughuli wanazofanya na  mchango wao kwa taifa” Amesisitiza.

Katika hatua nyingine Prof. Emanuel Mjema amesema kuwa chuo chake kiko katika hatua za mwisho za uanzishaji wa mafunzo ya Shahada ya Ualimu katika Biashara  ili kuziba pengo la uhaba wa walimu wa kufundisha masomo ya Biashara katika shule za Sekondari na vyuo kote nchini.

Amesema chuo chake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kimefikia uamuzi huo kufuatia  utafiti uliofanywa na jopo la wataalamu wa maandalizi ya Mtaala wa kufundishia programu hiyo mwaka 2012  uliobaini uwepo wa kiwango kikubwa cha uhitaji wa waataalam wa kufundisha masomo ya biashara wenye taaluma ya ualimu.

 “Sisi kama chuo cha Elimu ya Biashara tumeona uhitaji uliopo nchini wa kukosa wataalam wa kufundisha masomo ya Biashara wenye taaaluma ya ualimu ndio maana tumeamua kuanzisha  mtaala huu wa kufundishia wanafunzi wa Shahada ya Elimu katika Biashara ili  tupate wahitimu bora watakaofundisha wanafunzi wetu na kukidhi mahitaji ya soko” Amesisitiza.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof.Simon Msanjila akifafanua kuhusu  utafiti huo amesema kuwa Serikali itanufaika zaidi kutokana na kutambua mchango wa wafanyabiashara hao pindi itakapowaingiza katika mfumo rasmi.

Amesema wafanyabiashara hao wanapotembeza bidhaa zao barabarani, mitaani pamoja na maeneo mbalimbali ya miji hufanikiwa kusanya zaidi ya shilingi elfu thelathini kwa siku ( 30,000) jambo linalotia matumaini  kwa sekta ya biashara na Serikali iwapo watathaminiwa na kujengewa mazingira mazuri ya kutambuliwa.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

𝙂𝘼𝙈𝙊𝙉𝘿𝙄 𝙆𝘼𝘾𝙃𝙀𝙕𝘼 𝙆𝙄𝘽𝙄𝙉𝙂𝙒𝘼.