LOWASSA;NATAZAMWA NA CCM KILA KONA

Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara. Picha na Maktaba 
Dar es Salaam. Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa amesema anashindwa kujitokeza kuzungumzia au kufanya mambo yanayohusiana na urais kwa kuwa Kamati ya Maadili ya CCM inamfuatilia kwa karibu.
Alisema hayo jana alipoulizwa kuhusu kauli ya Rais Jakaya Kikwete wiki iliyopita akiwa Marekani ambako alielezea mafanikio na changamoto alizokumbana nazo wakati wa uongozi wake wa miaka 10.
Kikwete alisema: “Wakati unaingia Ikulu unakuwa na shauku kubwa pamoja na furaha ya ushindi, lakini hakika urais ni kadhia kubwa. Ukipata fursa ya kuwa rais kwa awamu mbili kama mimi nadhani zinatosha kabisa. Nimefanya mengi kwa nchi yangu atakayekuja ataendeleza nilipoishia.”
Kauli ya Lowassa inakuja ikiwa ni siku chache baada ya makada wengine wanaotajwa kuwania urais kupitia CCM kueleza maoni yao juu ya kauli hiyo ya Rais.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ameshalieleza gazeti hili kuwa kauli hiyo inampa hamasa kwa nia yake ya kutaka kuwania urais na kwamba alitangaza nia hiyo huku akifahamu kwa asilimia 100 uzito wa jambo hilo akisema kufahamu changamoto hizo ndiyo moja ya vitu vilivyomsukuma kuchukua uamuzi huo.
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisema: “Kama mtu ameamua kuwania nafasi hiyo ina maana anafahamu anachokitaka. Tunajua ziko changamoto na namna ya kukabiliana nazo, kwa hiyo hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi.”
Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla alisema: “Kauli kama hiyo haiwezi kumvunja mtu moyo, ari itabaki palepale tu kwa aliyetangaza nia. Aliyetangaza nia anataka kutoa utumishi wake kwa nchi yake kama mimi.”
Lowassa hajatangaza wazi nia hiyo zaidi ya kusema ameshawishika kuwania urais baada ya hivi karibuni, makundi mbalimbali kufika nyumbani kwake mjini Dodoma kumshawishi achukue fomu kuwania nafasi hiyo.
Miongoni mwa makundi yaliyojitokeza na kumshawishi pamoja na kumchangia fedha za kuchukua fomu ya kugombea urais ndani ya CCM ni pamoja na masheikh kutoka wilayani Bagamoyo, wachungaji wa makanisa ya Kipentekoste, wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na madereva bodaboda.
Msimamo wake hadi jana
Akizungumza jana wakati wa kuaga mwili wa Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Mohamed Mhita nyumbani kwa marehemu Oysterbay jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema: “Muda mwafaka ukifika nitatangaza nia na kuweka mikakati yangu wazi ili wananchi waijue. Kwa sasa siwezi kusema chochote kwa sababu ninatazamwa sana na chama. Ninachoweza kusema, siku nitakayotangaza nia, nitaeleza ni nini nitafanya kukabiliana na changamoto zote zilizopo Ikulu.
“Ninafahamu kuna changamoto nyingi, lakini siwezi kusema, subirini siku nitakapotangaza nia, nitaelezea ni kwa namna gani nitakabiliana na changamoto zilizopo katika ofisi hiyo nyeti nchini.”

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA