RAIS KIKWETE AHUDHURIA SHEREHE ZA KUMUAPISHA ASKOFU SANGU


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana Jumapili, Aprili 12, 2015 aliungana na maelfu ya waumini wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Shinyanga, kuhudhuria Ibada rasmi ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu mpya wa Jimbo hilo, Mhashamu Baba Askofu Liberatus Sangu.
Rais Kikwete aliwasili kwenye Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma, Ngokolo, mjini Shinyanga kiasi cha saa sita unusu mchana kwa ajili ya Ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na Maaskofu wakuu, maaskofu na maaskofu wasaidizi 38, akiwamo Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Rais wa Mabaraza ya Kipapa na Katibu Mwambata wa Uenezaji Injili Ulimwenguni Askofu Mkuu Protase Rugambwa kutoka Makao Makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican.
Askofu Sangu ambaye amewekwa wakfu na kusimikwa kwenye Siku ya Huruma ya Mungu Duniani anakuwa Askofu wa nne wa Jimbo la Shinyanga na anachukua nafasi iliyoachwa wazi tokea Novemba 6, 2012, wakati aliyekuwa Askofu wa Jimbo hilo, Baba Askofu Aloysius Balina alipofariki dunia.
Kwa miaka karibu mitatu, jimbo hilo limekuwa chini ya Usimamizi wa Kitume wa Askofu Mkuu Yuda Tadei R’uaichii wa Jimbo Kuu la Mwanza.
Askofu Sangu mwenye umri wa miaka 52 baada ya kuwa amezaliwa Februari 19, Mwaka 1963, katika Kijiji cha Mwazye, Jimbo Katoliki la Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, alipata daraja la upadrisho Julai 3, Mwaka 1994. Wakati anateuliwa na Baba Mtakatifu Francesco kuwa Askofu Februari 2, mwaka huu wa 2015, alikuwa na daraja la Mosinyori.
             Akikabidhi Jimbo hilo kwa Askofu mpya, Askofu Mkuu R’uaichii amesema kuwa Jimbo la Shinyanga ni moja ya majimbo makubwa zaidi ya Kanisa Katoliki nchini, likiwa na kilomita za mraba karibu 30,000 na waumini Wakatoliki wanaokaridiwa kufikia 300,000 katika Mkoa ambao idadi kiasi ya wakazi wake bado wanaamini  imani za jadi.
Amesema kuwa Jimbo hilo lina parokia 29, mapadre wa Jimbo 52, mapadre wa Kitawa 18 na hivyo kulifanya jimbo hilo kuwa na jumla ya mapadre 70 na “jeshi kubwa” la watawa 70.
Kwenye sherehe hizo zilizohudhuriwa na viongozi wengi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Ali Lufunga, Askofu Sangu amepewa zawadi ya sh. milioni 18, fimbo ya kiuchungaji na ng’ombe 10 wa maziwa na Wakatoliki wa Jimbo hilo.
Rais Kikwete alirejea Dar es Salaam jana jioni  baada ya kumalizika kwa Ibada hiyo.
Mwisho.

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.

13 Aprili, 2015

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.