NOOIJ AWEZA TUPIWA VIRAGO VYAKE JUMAPILI, MALINZI…


Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
HATIMA ya Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kuendelea na kazi au kupigwa chini, inatarajiwa kujulikana Jumapili (Mei 24, 2015).
Siku hiyo, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Rais wake, Jamal Malinzi inatarajiwa kukutana kujadili mwenendo, maandalizi na maendeleo ya timu za taifa.
Kikao hicho kinaitishwa siku moja baada ya Taifa Stars kutolewa Kombe la COSAFA kufuatia kufungwa mabao 2-0 jana na Madagascar katika mchezo wa Kundi B Uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
Safari imeiva; Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij anaweza kutupiwa virago Jumapili

Huo ni mchezo wa pili mfululizo timu hiyo kufungwa, baada ya awali kulala 1-0 mbele ya Swaziland Jumatatu na sasa itakamilisha ratiba Ijumaa kwa kumenyana na Lesotho kabla ya kurejea nyumbani.
Kikao hicho kinatarajiwa kuibuka na tamko la kumfuta kazi Nooij, kutokana idadi kubwa ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF.
Mholanzi huyo ameiongoza Stars katika mechi ya 15 jana tangu awasili mwishoni mwa Aprili kuchukua mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen ikifungwa sita, sare sita na kushinda tatu.
TFF ilihadaika na wasifu mzuri wa Nooij aliyetua Tanzania akitokea klabu ya St George ya Ethiopia Aprili mwaka jana na kumpa Mkataba mnono. 
Wasifu wa Nooij unasema amewahi kuwa mwalimu maalum katika programu za maendeleo ya soka katika Chama cha Soka Uholanzi (DFA) na pia amewahi kufundisha timu ya EVC 1913 ya Marekani na baadaye Kazakhstan.
Alikuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Burkina Faso katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2003 na mwaka 2004 alikuwa kocha wa muda wa klabu ya FC Volendam ya Uholanzi.
Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa kocha wa Msumbiji na akaiwezesha kufuzu kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza Mambas wanashiriki AFCON baada ya msoto wa miaka 12. 
Hata hivyo, katika fainali hizo, Msumbiji ilishika mkia katika kundi lake baada ya kuambulia sare moja na kufungwa mechi mbili. Baada ya kukosa tiketi ya AFCON 2012, Nooij akajiuzulu Septemba mwaka 2011 na nafasi yake kuchukuliwa na Mjerumani, Gert Engels.
Aprili 19 mwaka 2012, aliajiriwa na klabu ya Santos ya Afrika Kusini, ambako hata hivyo alifukuzwa Desemba 18, mwaka 2012 na kuhamia St George ya Ethiopia kabla ya kuja Tanzania Aprili mwaka jana. 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA