Serikali
imeuondoa muswada wa sheria ya haki ya kupata habari uliokuwa
uwasilisilishwe na kujadiliwa katika mkutano unaondelea wa bunge mjini
Dodoma.
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais (asiye na wizara maalum) Prof Mark Mwandosya
ameliambia bunge leo asubuhi kuwa serikali imefikia uamuzi huo kutokana
na maoni ya kamati ya kudumu ya bunge ya maendeleo ya jamiii iliyotaka
musawada huo uondolewe ili kutoa muda wa kujadiliwa na wadau.
Katika
taarifa yake hiyo kwa Bunge Mh. Mwandosya amewataka wadau wa habari
waendelee kutoa ushauri juu ya muswada huo pamoja na kuchangia maoni
zaidi ili kupata muswada ulio bora zaidi.
Prof
Mwandosya amesema muswada huo utawasilishwa na kujadiliwa katika mkutano
ujao wa bunge ambao utakuwa ni wa bunge la kumi na moja chini ya
serikali ya awamu ya tano.
Uamuzi
huo wa serikali umekuja kutokana na muswada huo kuzusha mgogoro na wadau
wa tasnia ya habari baada ya kuonekana kutowashirikisha wadau wa habari
moja kwa moja lakini pia kuonekana inaminya uhuru wa wananchi kupata
habari.
Wadau
mbalimbali wa habari wakiwemo chama cha wamiliki wa vyombo vya habari
MOAT wamekuwa wakilalamikia maudhui ya muswada huo kwa madai ya kuminya
uhuru wa vyombo vya habari pamoja na haki ya kupata taarifa kwa
wananchi.
Katika
mahojiano na mwanachama wa MOAT ambaye ni mwanzilishi mwenza wa mtandao
wa Jamii Forums jana Maxence Melo, alisema kuwa endapo muswada huo
ungepitishwa na kuwa sheria, basi tasnia nzima ya habari ingekufa kwa
kuwa umeweka njia ngumu ambazo hazitekelezeki katika upatikana wa
taarifa pamoja na mlolongo wa adhabu kali kwa wadau na waandishi
watakaokiuka sheria hiyo.
Naye
mwanasheria na mtafiti wa uchumi na biashara kutoka katika kituo cha
sheria na haki za binadamu Masud George alisema kuwa muswada huo ni
hatari kwa uchumi wa nchi kwani shughuli nyingi za kiuchumi zinategemea
upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati.
Aliongeza
pia kuwa, vyombo binafsi vya habari kama sehemu ya wawekezaji katika
sekta binafsi na chanzo muhimu cha ajira wanachangia kiasi kikubwa cha
uchumi wa nchi hivyo kuwadhoofisha ni kudhoofisha uchumi wa nchi
kiujumla
Comments