UJENZI WA KISIWA CHA KITALII WAANZA KATIKA ENEO LA MTONI MARINE KASKAZINI MAGHARIBI ZANZIBAR

 Sehemu  inayoendelea kufukiwa hapo Mtoni Marine ambayo itatumika hapo baadae kwa ajili ya eneo maalum litakalotoa fursa kwa Wananchi  kupata mapumziko.{ Public Beach }. 
 Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } Nd. Salum Khamis Nassor  akimueleza Balozi Seif  hatua zinazochukuliwa na Taasisi yake katika kuona taratibu za uwekezaji zinachukuliwa kwa wanaowekeza vitege uchumi vyao Nchini. 
Balozi Seif akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baghresa Group Bwana Said Salim wakitembelea kuona  mradi wa Ujenzi wa Majengo Mapya ya Hoteli ya Mtoni Marine ambayo iko chini ya Kampuni hiyo kwa hivi sasa.

MRADI mkubwa wa Kimataifa wa ujenzi wa kisiwa cha Kitalii  ambacho kitatengenezwa kwa mfumo wa ufukiaji Bahari umeanza rasmi katika eneo la Hoteli ya Utalii iliyopo Mtoni Marine kaskazini Magharibi ya Mji wa Zanzibar.

Hata hivyo gharama kamili za Mradi huo bado hazijafahamika  wakati utakapokamilika  rasmi ujenzi wake hapo baadaye.

Mradi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Kizalendo  ya Baghresa Group utahusisha ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa ya Ghorofa  Tano ya Daraja la Tano { Five Star + }, utengenezaji wa eneo la wazi la mapumziko { Public Beach } pamoja na kutengeneza  Kisiwa cha Mji mpya.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alishuhudia harakati za ujazaji wa mchanga katika eneo linalofukiwa ambazo hufanywa kwa utaalamu wa hali ya juu.

Mhandisi wa Mradi huo Bwana Ahmed Shamsi alimueleza Balozi Seif  kwamba chombo maalum kinachotumika kwa kazi ya uchimbaji wa mchanga Baharini  kina uwezo wa kunyonya  na kusafirisha mchanga kutoka ndani ya Bahari sambamba na kukata Majabali.

Mhandisi Shamsi alisema kazi hiyo inafanyika kwa saa 12 kila siku ambapo takwimu zinaonyesha wazi kwamba uchimbaji huo wa mchanga unaokwenda  zaidi ya mita 15 chini ya Bahari unafikia  Tani 600 za mchanga kwa saa Moja.

Alifahamisha kwamba harakati za uchimbaji na kufukia mchanga katika eneo hilo zilizoanza Mwezi uliopita wa Novemba zinatarajiwa kukamilika mwezi Januari mwaka ujao.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baghresa  Group  Bwana Said Salim Baghresa alisema kwamba ujenzi wa mradi huo muhimu kwa uchumi wa Nchi utasaidia mapato ya Taifa pamoja na kutoa ajira kubwa kwa vijana Wazalendo hapa Nchini.

Bwana Baghresa alisema mfumo wa ufukiaji Bahari kwa ajili ya kuanzisha miradi ya Kiuchumi ni mfumo unaotumiwa na Mataifa mbali mbali Duniani ambapo kwa Afrika  mradi kama tayari umeanza kutumiwa katika Kisiwa cha Seycheles.

Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Uongozi wa Baghresa Group kwa uamuzi uliochukuwa wa kuanzisha mradi huo mkubwa wa Kimataifa.

Balozi Seif alieleza kwamba kukamilika kwa mradi huo mkubwa  ambao umeshazoeleka katika Mataifa yaliyoendelea utasaidia kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla  Kiutalii Kimataifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi huo wa Baghresa Group kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila msaada unaohitajika katika  kuona mradi huo unafikia malengo uliojipangia.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamui wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/12/2015.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU