- Get link
- Other Apps
NA BASHIR YAKUB -
Mtu anapokufa huacha warithi wa namna mbalimbali. Yumkini ndani mwake waweza kuwamo watoto wenye umri mdogo na hata vichaa. Umri mdogo twaweza kuuhesabu kuanzia mwaka 0 mpaka 18. Aidha wakubwa ambao wamezidi miaka 18 hao nafasi yao inajulikana ikiwa marehemu ameacha mali.
Mali zao watakabidhiwa kwa utaratibu maalum ulioratibiwa na sheria. Swali litakuwa kwa watoto wadogo ambao hawawezi kukabidhiwa, tutahitaji kujua sheria inasemaje.
Hapa kuna mazingira ya aina mbili kwanza, ni pale marehemu anapoacha warithi watoto tu na hakuna mkubwa hata mmoja na pili ni pale anapoacha warithi wakubwa na watoto.
Pia kwa ufupi tutaangalia sheria inavyosema kuhusu mali za mrithi ambaye hana akili timamu. Hii nayo tutaangalia mazingira yote, mazingira anapokuwa na warithi wenzake na mazingira anapokuwa mrithi pekee.
1.MTOTO MDOGO.
Sura ya 352 kifungu cha 23 Sheria ya mirathi kinasema kuwa urithi au hati ya kusimamia mirathi haiwezi kutolewa kwa mtoto mdogo.
Tukiachana na hilo tujue kuwa ikiwa mtoto mdogo si mrithi pekee isipokuwa wapo ndugu zake wengine ambao ni warithi basi mmoja wao muadilifu atateuliwa kusimamia mirathi yote ikiwemo ya mtoto mdogo. Msimamizi huyo atakuwa na wajibu wa kuhakikisha anatunza mali ya mtoto/watoto hao mpaka wanakua na kuwa na uwezo wa kutunza mali zao binafsi.
Pili ni pale ambapo mtoto/watoto wadogo ndio warithi pekee wa mali yaani hakuna mkubwa kati yao. Ikiwa hilo litatokea basi mlezi wa watoto anaweza kuomba mahakamani kusimamia mirathi hadi watakapokua.
Taasisi ya udhamini ( trust cooperation) pia yaweza kuomba au kupewa bila kuomba jukumu la kusimamia mali za watoto hadi watakapokua. Hii ni kutoka kifungu cha 22 cha sheria ya mirathi. Yeyote atakayeteuliwa kati yao atakuwa na wajibu mkubwa wa kuhakikisha anatunza mali za watoto kwa kadri mahakama itakavyoelekeza.
Wakati mwingine wanaweza kujitokeza walezi wengi kila mmoja akitaka kusimamia mali za watoto. Ikiwa itakuwa hivyo basi suala hilo litapelekwa mahakamani na mahakama itaamua nani anafaa kusimamia mali hizo kwa kuzingatia zaidi mustakabali wa baadae ya hao watoto.
2. ASIYE NA AKILI TIMAMU.
Kifungu cha 23 cha sheria ya mirathi kinakataza kabisa mtu asiye na akili timamu kusimamia mali au kupewa hati ya kusimamia mirathi. Hii haijalishi hata katika mazingira ambayo yeye ndiye mrithi pekee.
Kifungu cha 37 cha sheria ya mirathi kinasema kuwa ikiwa mtu anayestahili kurithi au kusimamia mirathi hana akili timamu basi mali zake zitatunzwa na mtu ambaye anamtunza mtu huyo . Atasimamia mali hizo kwa maslahi ya mtu huyo. Isipokuwa kama kuna anayepinga kuhusu fulani kusimamia mali za asiye na akili timamu basi atapeleka maombi yake mahakamani na sababu kwanini anadhani fulani hafai katika hiyo nafasi.
Zaidi, msimamizi ataruhusiwa kutumia hela inayotoka katika mali zile kwa matumizi ya mtu huyo tu ikiwa kuna mali zinazozalisha. Matumizi ni kama mavazi, malazi, makazi, matibabu na mahitaji mengine muhimu kwa ustawi wa binadamu.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MWANDISHI WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI KILA JUMANNE. ”. 0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
Comments