Skip to main content

Mahakama yaidhinisha ushindi wa Kenyatta Kenya

Muhtasari

  1. Mahakama ya Juu Kenya imeamua uchaguzi wa marudio wa urais uliofanyika tarehe 26 Oktoba, 2017 ulikuwa halali.
  2. Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo baada ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kususia uchaguzi huo.
  3. Mahakama ya Juu ilikuwa imebatilisha uchaguzi wa kwanza uliokuwa umefanyika tarehe 8 Agosti ambapo Kenyatta alikuwa pia ametangazwa mshindi.

Habari za moja kwa moja

Kwa Picha: Kusherehekea uamuzi wa mahakama Nairobi

Mpiga picha wetu Peter Njoroge alipiga picha hizi za wafuasi wa Bw Kenyatta wakisherehekea karibu na majengo ya Mahakama ya Juu, Nairobi baada ya majaji kuidhinisha matokeo ya uchaguzi wa marudio uliofanyika tarehe 26 Oktoba.
Kusherehekea
BBC
Kusherehekea
BBC
Furaha
BBC
Kufurahia
BBC

IEBC yafurahishwa na uamuzi wa majaji

Tume ya Uchaguzi imefurahia uamuzi wa Mahakama ya Juu na kusema ni dhihirisho la kujitolea kwa tume hiyo kufanikisha uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika.
Imesema kupitia taarifa kwamba inasubiri uamuzi wa kina ambao utaiongoza katika kutathmini uchaguzi huo ulivyokuwa pamoja na mipango yake ya kuimarisha uchaguzi na tume yenyewe.

Hali ilivyokuwa nje ya Mahakama ya Juu

Mwandishi wetu Mercy Juma alikuwa nje ya majengo ya Mahakama ya Juu, Nairobi uamuzi wa kuidhinisha ushindi wa Kenyatta ulipotangazwa.
Tazama hali ilivyokuwa:

Ruto: Mungu amelikumbuka taifa

Naibu Rais William Ruto ameupokea uamuzi wa mahakama kwa furaha kubwa. Ameandika kwenye Twitter kwamba: "Halleluyah! Atukuzwe Mungu aliye mbinguni. Amelikumbuka taifa letu na kutupatia matumaini na mustakabali."
Ripoti

Kenyatta kuapishwa Jumanne kwa muhula wa pili

Rais Kenyatta sasa anatarajia kuapishwa kuwa Rais kwa muhula wa pili baada ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali kesi ambazo zilikuwa zinapinga ushindi wake katika uchaguzi wa marudio uliofanyika tarehe 26 Oktoba.
Kifungu 141(1b) cha Katiba ya Kenya kinasema Rais anafaa kuapishwa siku ya saba inayofuata siku ya kutolewa kwa uamuzi wa mahakama wa kuidhinisha uchaguzi iwapo kulikuwa na kesi iliyokuwa imewasilishwa.
Rais kwa mujibu wa katiba anafaa kuapishwa hadharani mbele ya Jjai Mkuu au Naibu Jaji Mkuu.

Maandamano yashuhudiwa ngome ya Odinga Kisumu

Maandamano yameshuhudiwa katika maeneo yenye wafuasi wengi wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
Katika mji wa Kisumu, magharibi mwa nchi hiyo, vijana wamejitokeza barabarani.
Video zimeonesha gari moja la kibinafsi likiteketea.

Wafuasi wa Kenyatta washerehekea kwa nyimbo

Wafuasi wa Kenyatta washerehekea uamuzi wa mahakama kwa nyimbo nje ya Mahakama ya Juu na katika maeneo mengine ambayo ni ngome yake.
Tazama:
Wengine wanasubiri Bw Kenyatta aapishwe:

Ekuru Aukot: Tumefurahishwa na uamuzi wa Mahakama

Mmoja wa waliogombea urais Ekuru Aukot amesema amefurahishwa na uamuzi wa mahakama ambayo alisema imedhihirisha uhuru wake na kujitolea kwake kudumisha sheria.
Amesema "wanasiasa hawawezi kuwa majaji na mahakimu."
" (Majaji wa Mahakama ya Juu) Walifanya hivyo 1 Septemba walipofuta ushindi wa Kenyatta, na wamerudia tena leo," amesema.
"Tunatumai kwamba sasa Kenya inaweza kusonga mbele, na wanaochochea ghasia kutokana na mzozo wa uchaguzi sasa hakuna mzozo tena baada ya uamuzi wa mahakama."
"Tunaweza sasa kuangazia mambo ya uzito zaidi. Chama chetu (Thirdway Alliance) sasa kutaangazia kuhakikisha Serikali inafanya kazi ipasavyo."

Duale: Wakati umefika kwa Wakenya kusonga mbele

Kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Aden Duale amesema wakati umefika sasa kwa Wakenya kusonga mbele.
Amesema Wakenya sasa wanafaa kuangazia kuungana pamoja, na amesema kuna njia nyingi za kuendeleza umoja.
"Wakenya walipiga kura na kumchangua Kenyatta, ushindi wake ulipingwa tena na leo tuna furaha kwamba kwa kufuata sheria, ushindi wa Kenyatta sasa umeidhinishwa kwa kauli moja," amesema.

HABARI ZA HIVI PUNDEMaraga: Majaji wameamua kesi zote hazina msingi

Maraga
AFP/Getty
Jaji Maraga amesema majaji kwa kauli moja wameamua kwamba kesi zote mbili hazina msingi.
Kesi ya Bw Harun Mwau na wanaharakati wawili Njonjo Mue na Khelef Khalif zimetupiliwa mbali.
Uchaguzi wa 26 Oktoba umedumishwa, sawa na ushindi wa Bw Kenyatta. Kila upande utasimamia gharama yake..
Uamuzi wa kina utatolewa katika kipindi cha siku 21.

Maraga: Kesi ya pili ilihusu utaratibu na uhalali wa uchaguzi

Mgombea akijiondoa kabla ya uchaguzi, matokeo yake ni gani? Kuna mgombea aliyejiondoa kikamilifu?
IEBC na mwenyekiti wake waliandaa uchaguzi kwa kufuata Katiba na sheria za uchaguzi?
Uchaguzi wa 26 Oktoba ulitimiza viwango vya katiba vya uchaguzi huru na wa haki?
Matokeo ya kutofanyika uchaguzi maeneo mengine kunaathiri uchaguzi?
Uchaguzi uliathiriwa na visa vya udanganyifu?
Marekebisho ya sheria yaliyoidhinishwa Oktoba yanaathiri chochote, yalifuata sheria?

Maraga: Kesi moja ilihusu uteuzi wa wagombea

Jaji anaangazia kesi ya kwanza ambayo amesema ilihusu uteuzi wa wagombea wa urais, iwapo uteuzi wa wagombea ulifaa kufanywa upya wakati wa uchaguzi mpya na iwapo muda ufaao ulifaa kufuatwa.

Maraga: Hatutasoma uamuzi wa kina

Jaji Mkuu amesema Majaji hawakuwa na muda wa kuandika uamuzi wa kina, hivyo watasoma uamuzi kwa muhtasari.

Maraga: Kesi zote mbili ziliungwanishwa

Jaji Maraga anafafanua kuhusu kesi zilizokuwa zimewasilishwa. Zilikuwa mbili lakini zikaunganishwa na kusikilizwa kwa pamoja.

Majaji wa Mahakama ya Juu waingia ukumbini

Majaji wa Mahakama ya Juu wameingia katika ukumbi wa Mahakama. Kikao sasa kinatarajiwa kuanza.

Mambo muhimu yatakayoangaziwa na majaji

Katika Kesi majaji watatakiwa kutoa uamuzi kuhusu masuala yafuatayo:
  • Iwapo tume huru ya taifa ya chaguzi na mipaka (IEBC ) ilifaa kuteuwa upya wagombea urais au la.
  • Uamuzi pia utatolewa na mahakama hiyo juu zaidi juu ya ya ikiwa kujiondoa kwenye uchaguzi huo kwa mgombea wa upinzani Raila Odinga.
  • Majaji pia watatoa uamuzi kuhusu ikiwa baada ya tume ya IEBC kushindwa kuendesha uchaguzi katika ameneo bunge 25 kati ya 290 kunahalalisha ama kubatilisha matokeo ya uchaguzi.
  • Aidha Mahakama hiyo itawaeleza waKenya ikiwa tume ya uchaguzi (IEBC) ilikuwa na uwezo wa kuandaa uchaguzi wa haki na huru baada ya kugubikwa na mgawanyiko miongoni mwa wajumbe wake.
  • Kwa upande mwingine Wakenya watasubiri kusikia uamuzi wa mahakama kuhusu kama ghasia zilizotokea kabla na baada ya uchaguzi wa marudio wa urais ziliathiri ama hazikuathiri matokeo ya uchaguzi na kuufanya kuwa usio wa haki na huru au la.
  • Mahakama itatoa ufafanuzi juu ya dosari ya karatasi za kupigia kura, maarufu kama form 34A ziliathiri matokeo ya uchaguzi.
  • Hukumu hii inasubiriwa kwa shauku kubwa na raia wa Kenya pamoja na kwingineko duniani, huku wengio wakijiuliza hatma ya Kenya.

Ulinzi waimarishwa nje ya Mahakama ya Juu

Ulinzi umeimarishwa nje ya majengo ya Mahakama ya Juu na katika maeneo mengine katika jiji la Nairobi majaji wakitarajiwa kutoa uamuzi kuanzia saa nne asubuhi.
Uamuzi huo ni wa pili kutolewa na mahakama hiyo baada ya uamuzi wa tarehe 1 Septemba ambapo mahakama hiyo ilibatilisha uchaguzi wa kwanza uliofanyika tarehe 8 Agosti.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga alisusia uchaguzi huo wa marudio.

Hujambo!

Hujambo na karibu kwa taarifa za moja kwa moja kuhusu kutolewa kwa uamuzi wa Mahakama ya Juu Kenya kuhusu uchaguzi wa marudio wa urais uliofanyika tarehe 26 Oktoba, 2017.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.